Raila agutushwa na mabadiliko katika ripoti ya BBI

Rais Uhuru Kenyatta atia saini wakati wa hafla ya kuzindua saini za kufanikisha ripoti ya BBI. (Picha PSU)
Rais Uhuru Kenyatta atia saini wakati wa hafla ya kuzindua saini za kufanikisha ripoti ya BBI. (Picha PSU)

 Rais Uhuru Kenyatta siku ya Jumatano alizindua ripoti ya mwsho ya BBI iliyokuwa imefanyiwa mabadiliko ambayo kiongozi wa ODM Raila Odinga alionekana kutofahamu.

Mswada huo mpya unalenga kubuni maeneo bunge mapya 70 katika kaunti 28. Inaruhusu kuteuliwa kwa wanawake katika bunge la kitaifa na katika mabunge ya kaunti lakini ni wale pekee waliogombea nyadhifa hizo katika uchaguzi watakao teuliwa.

Kipau mbele kitapewa wanawake waliozoa kura nyingi ili kutamatisha mazoea ya wanasiasa kuwatunuku “wapenzi” wao nyadhifa za uteuzi.

Marekebisho hayo ya katiba pia yanapendekeza kuimarisha mamlaka ya seneti na kuwapa wakilishi wadi nafasi pia kuhudumu kama mawaziri katika kaunti.

Mapendekezo hayo pia yanampa rais mamlaka ya kuwateua manaibu waziri 14 kutoka bunge la kitaifa.

Mswada huo hata hivyo umeondoa baadhi ya vipengele ambavyo vilikuwa vimezua utata wa kisiasa.

Moja wapo ya mapendekezo yaliondolewa ni vyama vya kisiasa kuteua makamishna wa tume ya uchaguzi na mipaka na kubuniwa kwa baraza la polisi.

Mswada huu mpya pia hauzungumzii kufurushwa kwa makamishna wa sasa wakiongozwa na mwenyekiti Wafula Chebukati.

Cha kushangaza ni kwamba kinara wa upinzani Raila Odinga alionekana kutofahamu baadhi ya mabadiliko katika mswada wa mwisho. Alikuwa ameisifia BBI kwa kuruhusu vyama vya kisiasa kuteua makamishna wa tume ya IEBC.

Pendekezo hilo hata hivyo liliondolewa kutoka mswada wa mwisho na kuibua maswali ikiwa Raila alikuwa amejulishwa kuhusu mabadiliko hayo.

Katika hotuba yake, Raila alipigia debe vyama vya kisiasa kuchagua makamishna wa IEBC, mapendekezo ambayo Raila amekuwa akiyaunga mkono.

Kinara huyo wa upinzani alikuwa amesifia uchaguzi wa mwaka 2002, uliyosimamiwa na makamishna 20 walioteuliwa na vyama vya kisiasa.

Pendekezo la kuipa Kaunti ya Nairobi hadhi maalum pia limeondolewa na sasa kaunti hiyo itasalia tu kama kaunti zingine.

Hatua hii inamaanisha kwamba gavana wa Nairobi atakuwa na mamlaka kamili ya gavana baada ya kukamilika kwa muda wa kuhudumu wa NMS.

Seneti sasa itakuwa na mamlaka ya kuwapiga msasa mdhibiti wa bajeti na tume ya vijana miongoni mwa majukumu mengine mapya.