Chuma cha Sonko ki motoni, hoja ya kumfurusha yawasilishwa

Muhtasari

• Hoja iliwasilishwa bungeni na kiongozi wa wachache Michael Ogada.

• Hoja hiyo iliyotiwa saini na takriban wawakilishi wadi 86

• Ogada anataka Sonko kubanduliwa ofisini kwa sababu kadhaa zikiwemo matumizi mabaya ya mamlaka na ufisadi.

Gavana wa Nairobi Mike Sonko, anayekabiliwa na hoja ya kutokuwa na imani naye.
Gavana wa Nairobi Mike Sonko, anayekabiliwa na hoja ya kutokuwa na imani naye.

Masaibu ya gavana wa Nairobi Mike Sonko yanazidi kukithiri huku hoja ya kutokuwa na imani naye ikiwasilishwa kwa bunge la kaunti ya Nairobi.

Hoja hiyo iliyotiwa saini na takriban wawakilishi wadi 86 iliwasilishwa bungeni na kiongozi wa wachache Michael Ogada.

Ogada ambaye pia ni mwakilishi wadi wa Kileleshwa anataka Sonko kubanduliwa ofisini kwa sababu kadhaa zikiwemo matumizi mabaya ya mamlaka na ufisadi.

Akiwasilisha hoja hiyo Ogada aliambia kikao cha  bunge la kaunti ya Nairobi siku ya Alhamisi kwamba Sonko amekuwa mgeni wa kila siku wa mahakama  kujibu mashtaka ya ufisadi na matumizi mabaya ya mamlaka na kwa hivyo hafai kuendelea kuhudumu kama gavana.

Siku ya Alhamisi Sonko anasemekana kuitisha mkutano wa dharura na wakilishi wadi wanaomuunga mkono kupanga mikakati ya kuangusha hoja hiyo.

Wakilishi wadi wanaomuunga mkono Sonko walidai kwamba hoja ya kutokuwa na imani naye imechochewa na hatua ya gavana huyo kukataa kutia saini mswada wa shilingi bilioni 37.5 wa bajeti ya 2020 – 21.

Walidai kwamba uamuzi wa kumuondoa Sonko uliafikiwa katika mkutano wa Capital Hill siku ya Jumanne uliyohudhuriwa na uongozi wa bunge la kaunti.

Waliohudhuria mkutano huo hata hivyo walishikilia kwamba ulikuwa kuhusu mchakato wa BBI.

Uongozi wa Sonko katika kaunti ya Nairobi umekuwa na changamoto za aina yake huku gavana huyo akihudumu kwa takriban miaka miwili sasa bila naibu gavana tangu kujiuzulu kwa Polycarp Igathe mwaka 2018 miezi michache tu baada ya kuapishwa.  

Igathe alitaja mazingira duni ya kufanya kazi na gavana Mike Sonko kama sabau zake kuu kujiuzulu. Shinikizo za kumtaka Sonko kumteua naibu gavana zimeambulia patupu huku wakati mmoja akipendekeza wakili Miguna Miguna ambaye anakaa nchini Canada kuwa naibu wake.

Sonko pia alitia saini mkataba kusalimisha baadhi ya idara muhimu za kaunti kuwa chini ya usimamizi wa serikali ya kitaifa.