Itumbi aambulia patupu katika kesi dhidi ya Matiang'i

Waziri wa mambo ya ndani Fred Matiang'i (kushoto) na Dennis Itumbi
Waziri wa mambo ya ndani Fred Matiang'i (kushoto) na Dennis Itumbi

Mahakama ya kukabiliana na ufisadi imetupilia mbali ombi la mwanablogi Dennis Itumbi aliyetaka kumshtaki waziri wa mambo ya ndani Fred Matiang’i.

Itumbi alitaka Matiang’i afunguliwe mashtaka ya ufisadi kuhusiana na ardhi yenye utata ya Ruaraka.

Hata hivyo, siku ya Ijumaa, hakimu Douglas Oguti wa mahakama ya kukabiliana na ufisadi alisema kwamba Itumbi alikosa kueleza vile alipata taarifa au stakabadhi alizoweka katika hati yake ya kiapo dhidi ya Matiang’i.

"Hati yake ya kiapo haina maelezo kuonyesha kama alikuwa na idhini kutumia stakabadhi za umma na ni lini au alipata vipi stakabadhi hizo," alisema hakimu Oguti.

"Kwa sababu alikosa kueleza vile alipata stakabadhi hizo, haziwezi kutumika mahakamani. Anapaswa kuwa ameeleza vile alipata stakabadhi hizo za umma na zingine kabinafsi."

Miongoni mwa stakabadhi hizo ni barua zilizoandikwa na hazina ya kitaifa, kamishna wa ardhi na wizara ya elimu.

Itumbi hakuwa na stakabadhi zenye mhuri maalum wa serikali.

Mahakama pia ilieleza kwamba Itumbi hakuthibitisha hatua yoyote ya kutaka ruhusa kutoka idara husika kuomba apewe stakabadhi hizo.

Stakabadhi hizo pia hazikuwa zimetiwa saini.

"Stakabadhi hizi vile zilivyo haziafikii vigezo vya sheria na haziwezi kuwasilishwa au kutumika mahakamani."

"Stakabadhi haziafikii sheria kuhusu ushahidi mahakamani".