Democrats wataka Trump kuondolewa madarakani mara moja

Maafisa wa usalama wakikabiliana na waandamanaji katika bunge la Congress Marekani
Maafisa wa usalama wakikabiliana na waandamanaji katika bunge la Congress Marekani

Wapinzani wa Rais wa Marekani Donald Trump katika mabunge yote mawili wametoa wito wa rais huyo kuondolewa madarakani baada ya wafuasi wake waliokuwa wakifanya vurugu kuvamia bunge.

Seneta wa Democratic Chuck Schumer amesea Bwana Trump anastahili kuondolewa mara moja. Na ikiwa sio hivyo, Spika wa bunge la Wawakilishi Nancy Pelosi amesema anaweza kupigiwa kura ya kutokuwa na imani naye.

Kuondolewa kwa rais huyo kupitiamuswada wa kutokuwa na imani naye, kutahitaji kuungwa mkono na wabunge wa Republican ambao kufikia sasa ni wachache tu wanaoonekana kutofautiana naye.

Katika hotuba iliotumwa kwa njia ya video, Bwana Trump alisema amejitolea kukabidhi mamlaka kwa amani.

Rais huyo alisema utawala mpya utaapishwa Januari 20 na kutoa wito wa "maridhiano".

Pia alisema, "hasira imesababishwa na vurugu, uasi wa sheria na ghasia" zilizotokea Jumatano na kwamba "hasira lazima zitulizwe". Video hiyo ilishirikishwa kwenye akaunti yake ya Twitter, ambayo iliwezeshwa tena kutumika kuanzia Alhamisi baada ya kufungwa kwa muda kwasababu ya tukio la uvamizi wa bunge.

Watu wanne walifariki dunia wakati wa uvamizi huo huku wengine 68 wakiwa wamejeruhiwa.

Sasa hivi maafisa wa polisi wameanza kuchunguzwa jinsi walivyoshughulikia maandamano hayo na kukosolewa kwa kushindwa kusitisha waandamanaji kuvunja sheria na kuingia bungeni.

Maafisa waliokuwa walinda usalama katika Bunge la Wawakilishi ikiwa ni pamoja na muongozaji shughuli za bunge wamejiuzulu.

Taarifa zinasema mkuu wa polisi bungeni Steven Sund pia naye anajiuzulu kuanzia Januari 16 kufuatia wito uliotolewa na Bi. Pelosi.

Bwana Schumer upande wake anataka wenzake wa bunge la Seneti kufutwa kazi.

Waziri wa usafirishaji Elaine Chao ndio wa hivi karibuni kujiuzulu katika utawala wa Trump kwasababu ya maandano hayo.

Maafisa kadhaa wa ngazi ya chini pia wamejiuzulu.

Rais mteule Joe Biden amesema: "Hivi unasema kama hapo jana ingekuwa ni maandamano ya kundi la Black Lives Matter hatua zilizochukuliwa dhidi yao hazingekuwa tofauti kabisa ikilinganishwa na walivyochukuliwa wahuni waliovamia bunge."

Rais mteule wa Marekani Joe Biden na rais anayeondoka Donald Trump.
Rais mteule wa Marekani Joe Biden na rais anayeondoka Donald Trump.

Wabunge wasema nini?

Idadi ya wabunge kadhaa wanataka Bwana Trump aondolewe kama rais. Wengi wao wakiwa ni kutoka chama cha Democratic hata hivyo, wachache wa Republican wanaunga mkono hatua hiyo.

"Rais huyu hastahili kuendelea kushika hatamu hata kwa siku moja zaidi," amesema Bwana Schumer, ambaye ataongoza chama cha Democratic chenye wabunge wengi katika Bunge la Seneti litakapoanza kikao kipya baadaye mwezi huu.

Amesihi baraza la Bwana Trump kumuondoa madarakani kwa kutumia marekebisho ya 25 ya katiba ya Marekani, ambayo yanaruhusu makamu rais kuchukua uongozi ikiwa rais ameshindwa kutekeleza majukumu yake kwasababu ya matatizo ya kiakili au kimwili.

Hatua hiyo itamhitaji makamu rais Mike Pence na angalau wabunge wanane wa baraza la mawaziri kumpinga Trump na kutekeleza kifungu hicho cha katiba hatua ambayo hadi kufikia sasa imeonekana kutokuwa tayari kutekelezwa.

Bi. Pelosi amemuelezea Trump kama "mtu hatari" na kusema: "Hii ni hali ya dharura mno." Inayohitaji kushughulikiwa kwa haraka.

Na aliwacha wazi uwezekano wa kupiga kura ya kutokuwa na imani naye ikiwa wabunge wanaomuunga mkono Bwana Trump hawataweza kuanza mchakato wa kifungu cha 25 cha katiba.

Hata hivyo, Democrats watahitaji uungwaji mkono kutoka kwa Republicans kupata idadi stahiki kisheria katika bunge la seneti ambayo ndio wengi angalau thuluthi mbili kumuondoa Trump madarakani chini ya kifungu cha kutokuwa na imani naye ambapo itakuwa vigumu kufikia idadi hiyo.

Polisi waliwajibika vipi?

Polisi wamekosolewa vikali kwa jinsi walivyoshughulikia ghasia hizo.

Picha zilizonaswa ndani ya bunge zilionesha vile waandamanaji walivyokuwa wanaingia katika baadhi ya sehemu za bunge bila kuzuiliwa na yeyote.

Mmoja wao alionekana akiingia katika ofisi ya Spika Pelosi na kuweka muguu yake juu ya dawati lake.

Mkuu wa polisi pia amepewa likizo ya lazima baada ya mwanamke mmoja kupigwa risasi hadi kufariki duniani katika sakafu ya bunge la wawakilishi.

Mwanamke huyo amesemekana kwamba alikuwa wanajeshi.

Ashli Babbitt, 35, ni sehemu ya walioingia bungeni wakati mjadala wa kuidhinisha ushindi wa Bwana Biden ukiwa unaendelea.

Polisi imesema pia watu watatu Benjamin Philips, 50 kutoka Pennsylvania; Kevin Greeson, 55, kutoka Alabama; na Rosanne Boyland, 34, kutoka Georgia - walifariki dunia wakendelea kupata huduma ya kwanza.

Familia ya Greeson inasema jamaa yao alifariki dunia kwa mshtuko wa moyo.

Shirika la Ujasusi linatafuta waliohusika na vurugu hizo.