Mshukiwa wa mauaji ya Kiambu akiri kuchochewa na kipindi 'Killing Eve'

Gari lililobeba miili ya wahasiriwa 4 wa mauaji katika kijiji cha Karuri, Kiambaa, Kiambu, Januari 6, 2020.
Gari lililobeba miili ya wahasiriwa 4 wa mauaji katika kijiji cha Karuri, Kiambaa, Kiambu, Januari 6, 2020.
Image: ANDREW KASUKU

Mshukiwa mkuu wa mauaji ya kinyama ya watu watano wa familia moja katika eneo la Kiambu  anasema alichochewa na kipindi cha Runinga ya Uingereza  - Killing Eve.

Killing Eve  ni kipindi cha ucheshi kinachopendwa sana nchini Uingereza.

Lawrence Simon Warunge aliwaambia polisi kwamba alienda mtandaoni kutafuta jinsi anavyoweza kutekeleza njama zake vile mhusika mkuu katika filamu psychopathic assassin Villanelle hufanya bila athari yoyote.

"Anasema alitafuta maelezo yote mtandaoni na alikusudia kuficha njia zake na hata kuwaua dada zake waliobaki," afisa wa upelelezi alisema.

Lawrence mwenye umri wa miaka 23, na mwanafunzi wa teknolojia ya wasiliano katika chuo kikuu na rafikiye wa kike Sarah Muthoni, walifikishwa kortini Jumatatu ambapo polisi waliomba muda zaidi wa kumshikilia hadi watakapomaliza uchunguzi wao wa mauaji hayo.

Polisi wanashangaa jinsi mvulama huyo alivyofanikiwa kuwaua watu hao watano bila upinzani.

Kuna mipango kufanyia upasuaji miili hiyo ili kubainisha kilichosababisha vifo vyao.

Alikamatwa Ijumaa usiku katika eneo la Kabete baada ya kwenda mafichoni.

Babake na mamake Lawrence walikuwa miongoni mwa watu 5 aliyoua katika eneo la Karura, kaunti ya Kiambu Jumanne iliyopita.

Polisi walisema walimkamata Lawrence baada ya kutoweka tangu Jumanne wakati wazazi wake, ndugu zake wawili, na mfanyakazi waliuawa kinyama nyumbani kwao katika kaunti ya Kiambu.

Baada ya kukamatwa, alikiri tukio hilo na kuwaongoza polisi kwenye makazi katika eneo la Mai Mahiu Jumamosi ambapo walipata silaha ya muuaji- kisu cha jikoni, kipande cha nguo, viatu, na karatasi.

Polisi walichimba ukuta wa choo na walitumia kamba kupata vifaa vingine kutoka kwenye shimo lenye kina cha futi 20.

Pia aliwapeleka polisi kwenye uwanja wazi katika eneo hilo hilo ambapo alisema aliteketeza baadhi ya ushahidi.

Lawrence anadai kuwa aliwaua hao watano peke yake, lakini polisi walisema kuna uwezekano alishirikiana na washukiwa wengine.

Sehemu ya kutisha zaidi ni pale Lawrence alisema alipata baba yake-Nicholas Njenga Warunge akijaribu kutoroka na kuvunjika mguu baada ya kuruka kutoka ghorofani.

"alisema baba alitegwa na kebo ya umeme wakati akikimbia na kuruka kutoka kwenye ghorofa na akazidiwa zaidi baada ya kuvunjika mguu. Hii ilimpa Lawrence wakati wa kumshika na kumuua kama nyoka, ”afisa mmoja wa polisi alisema.

Mwili wa babake ulikuwa na majeraha 34 ya kudungwa kisu.

Lawrence alisema baada ya kuwaua hao watano akitumia kisu cha jikoni saa nane hivi alitumia pikipiki kwenda hadi kituo cha kibiashara cha Wangige ambapo alipanda gari na kwenda Mai Mahiu akiwa amebeba silaha alizokuwa ametumia kutekeleza mauaji na ushahidi mwingine.