Mshukiwa wa mauaji ya wakili Koki kuzuiliwa siku 14

Mshukiwa wa mauaji ya wakili Elizabeth Koki, Christian Kadima alifikishwa katika mahakama ya Mavoko siku ya Jumatatu.
Mshukiwa wa mauaji ya wakili Elizabeth Koki, Christian Kadima alifikishwa katika mahakama ya Mavoko siku ya Jumatatu.
Image: GEORGE OWITI

Mshukiwa katika mauaji ya wakili Elizabeth Koki siku ya Jumatatu  alifikishwa katika mahakama ya Mavoko.

Christian Kadima hakuruhusishwa kula kiapo kwa sababu upande wa mashtaka uliomba siku 14 zaidi kukamilisha uchunguzi wao.

Hakimu mkuu Benard Kasavuli alikubali ombi la upande wa mashtaka kupewa muda wa majuma mawili kukamilisha uchunguzi.

Mshukiwa hakupinga ombi hilo.

Marehemu wakili Elizabeth Koki.
Marehemu wakili Elizabeth Koki.
Image: CORAZON WAFULA

Uchunguzi huo utajumuisha kubaini jina halisi la mshukiwa na maovu ambayo anadaiwa kutekeleza.

Ataendelea kuzuiliwa katika kituo cha polisi cha Mlolongo..

Kesi hiyo itatajwa Januari 25.

Kadima alitiwa mbaroni kwa madai ya kumuua Koki, 32, katika nyumba yake mtaani Syokimau, kaunti ya Machakos siku ya Alhamisi.

Kamanda wa polisi wa Athi River George Kashimiri katika eneo la tukio mtaani Syokimau, kaunti ya Machakos, January 9, 2021.
Kamanda wa polisi wa Athi River George Kashimiri katika eneo la tukio mtaani Syokimau, kaunti ya Machakos, January 9, 2021.
Image: CORAZON WAFULA

Alikamatwa na kuzuiliwa katika kituo cha polisi cha mlolongo Ijumaa usiku.

Marehemu alikuwa mmoja wa wamiliki wa kampuni ya uawakili ya ‘Githinji and Koki Advocates’ na aliendesha shughuli zake mjini Nairobi.

 

Maafisa wa DCI wanaochunguza mauaji hayo walisema mshukiwa alikamatwa katika chumba cha kukodisha juma la Rosta House  mjini Nairobi mwendo wa saa tano usiku baada ya kutoroka eneo la tukio.

Walisema gari la marehemu ambalo mshukiwa alitumia kutoroka, Volkswagen KCQ 999 K lilipatikana katika jumba la Marsabit kwenye barabara ya  Ngong.

Alikuwa amepena mtu gari hilo kulirejesha kwa familia ya marehemu.

Boma la wakili Elizabeth Koki eneo la Katani, kaunti ya Machakos Januari 9, 2021.
Boma la wakili Elizabeth Koki eneo la Katani, kaunti ya Machakos Januari 9, 2021.
Image: CORAZON WAFULA

Maafisa wa DCI pia walisema kwamba jamaa huyo raia wa kigeni hakuwa na stakabadhi za usafiri wakati alipokamatwa.

Afisa mkuu wa DCI katika kaunti ya Machakos Charles Mutua alisema kwamba mwili wa marehemu ulikuwa na alama za kunyongwa.

Pia kulikuwa na damu kwa kitanda chake.