Amerika yajiondoa kutoka uangalizi wa uchaguzi wa Uganda

Balozi wa Amerika nchini Uganda Natalie Brown
Balozi wa Amerika nchini Uganda Natalie Brown
Image: HISANI

Amerika haitashiriki katika uangalizi wa uchaguzi wa Uganda siku ya Alhamisi, Balozi Natalie Brown amesema.

Kupitia taarifa siku ya Jumatano, Balozi wa Amerika nchini Uganda alisema kujiondoa kumechangiwa na uamuzi wa Tume ya Uchaguzi ya Uganda kukataa kuidhinisha zaidi ya asilimia 75 ya waangalizi wa uchaguzi wa Amerika.

"Huku asilimia 15 tu wakiwa wamepewa idhini, haiwezekani kwa Amerika kutazama shughuli za uchaguzi wa Uganda katika maeneo ya kupigia kura kote nchini," Brown alisema.

 

Alisema kuwa licha ya maombi mengi, Tume ya Uchaguzi haikutoa ufafanuzi wa uamuzi wake,"ambao uliwasilishwa siku chache kabla ya uchaguzi".

Brown alibaini kuwa walikuwa wamefuata mahitaji yote ya idhini ya Tume ya Uchaguzi, kama walivyofanya katika uchaguzi uliopita nchini Uganda.

"Madhumuni ya uchunguzi wa kidiplomasia wa uchaguzi ni kuonyesha nia yetu katika mchakato wa uchaguzi huru, wa haki, amani, na umoja," alisema.

"Waangalizi wa kidiplomasia sio washiriki au washauri katika mchakato wa uchaguzi. Badala yake, wanafuatilia kwa utaratibu mwenendo wa uchaguzi, kufuata viwango vikali vya kutopendelea, kutokuingilia, na kufuata sheria za nchi husika."

Alisema kuwa Amerika inaunga mkono mchakato wa uchaguzi huru, wa haki, amani, na umoja.

Katika uchaguzi wa Uganda wa 2016, Ujumbe wa Ammerika ulituma waangalizi wa uchaguzi wa kidiplomasia 88.

Aliongeza wana wasiwasi kuhusu ripoti kwamba Tume ya Uchaguzi ilikuwa imekataa maombi ya idhini kutoka kwa wanachama wa ujumbe mwingine wa kidiplomasia na idadi kubwa ya waangalizi wa Uganda.

 

"Asasi nyingi za kiraia zilipanga kuangalia uchaguzi, lakini wengi hawajasikia tena kutoka kwa Tume ya Uchaguzi juu ya maombi yao ya idhini."

Brown alisema kwa kukosekana kwa waangalizi, haswa waangalizi wa Uganda ambao wanawajibika kwa raia wenzao, uchaguzi wa Uganda utakosa uwajibikaji, uwazi na ujasiri ambao ujumbe wa waangalizi unatoa.