Uganda yaagiza mitandao yote ya kijamii kufungwa

Image: GETTY IMAGES

Uganda imeagiza watoaji huduma za mtandao kufunga mitandao yote ya kijamii na programu za kutuma ujumbe kufikia Jumanne hadi wakati usiojulikana, kwa mujibu wa barua kutoka kwa mdhibiti wa mawasiliano nchini humo iliyonukuliwa na shirika la habari la Reuters.

Watumiaji walikuwa wamelalamika awali Jumanne, kwamba hawaweza kupata mtandao wa Facebook na WhatsApp, majukwaa ya mitandao ya kijamii inayotumiwa sana katika kipindi cha kampeni kabla ya uchaguzi wa urais kwenye nchi hiyo ya Afrika Mashariki.

Tume ya mawasiliano Uganda inaagiza kusitisha ufikiwaji na utumiaji, wa moja kwa moja au kinyume chake, kwa mitandao yote ya kijamii pamoja na programu za kutuma ujumbe mitandaoni hadi siku isiyojulikana," Barua kutoka kwa mkurugenzi mkuu wa tume imesema hivyo kwa watoaji huduma za mtandao.

Msemaji wa tume hiyo Ibrahim Bbossa na msemaji wa serikali Ofwono Opondo hawakujibu simu walizokuwa wanapigiwa ili kutoa maoni yao kuhusiana na hilo.

Afisaa katika Wizara ya Habari Judith Nabakooba alisema hakuweza kusema chochote kwa wakati huo.

Chanzo katika sekta ya mawasiliano Uganda, kimesema serikali ilikuwa imeweka wazi kwa wakuu wa kampuni za mawasiliano kuwa kupiga marufuku mitandao ya kijamii ilikuwa ni kujibu hatua iliyochukuliwa na mtandao wa Facebook ya kufunga baadhi ya akaunti zinazounga mkono serikali.

Mtandao huo mkubwa wa mawasiliano wa Marekani ulisema Jumatatu, umeamua kuchukua hatua ya kufunga mawasiliano kwa mtandao unaohusishwa na wizara ya habari Uganda kwa kutumia akaunti za uongo na kutengeneza nakala zaidi ya moja kuweka ujumbe wao kabla ya uchaguzi unaofanyika wiki hii.