Wafuasi wa Gideon Moi waponea kichapo katika mkutano wa Ruto

Muhtasari

• Polisi walilazimika kuingilia ili kuwaokoa wafuasi wa Gideon kutokan gadhabu ya mashabiki wa Ruto.

Polisi waingilia kati kutuliza hali wakati wa mkutano wa Naibu Rais William Ruto katika eneo Kabarnet, Baringo, siku ya Jumamosi.
Polisi waingilia kati kutuliza hali wakati wa mkutano wa Naibu Rais William Ruto katika eneo Kabarnet, Baringo, siku ya Jumamosi.
Image: JOSEPH KANGOGO

Wafuasi wa Seneta Gideon Moi siku ya Jumamosi waliponea maisha wakati wa ziara ya Naibu Rais William Ruto katika mji wa Kabarnet, Baringo.

Ruto alikuwa akihutubia umati wakati wafuasi wa Gideon walipovamia mkutano wakiwa wamebeba mabango yaliyokuwa na picha zake. Mabango hayo yaliandikwa 'Gideon Tosha'.

'Waueni' watu wengine walisikika wakipiga kelele huku wakiwanyeshea mijeledi na mateke wafuasi wa Gideon walipokuwa wakiwafukuza na kung'oa mabango.

 

Polisi walilazimika kuingilia ili kuwaokoa wafuasi wa Gideon kutokan gadhabu ya mashabiki wa Ruto.

"Gideon hajawahi kujishughulisha nasi wakati mgumu wa njaa, mashambulizi ya ujambazi, mafuriko na Covid-19, kwa hivyo hatumtambui kabisa," MCA wa Bartabwa Reuben Chepsongol alisema.

Aliungwa mkono na mwenzake wa Tenges Silas Tochim, ambaye alimtaja Gideon kama seneta wa 'hayupo'.

Naibu rais William Ruto akihutubia wananchi katika eneo la Kabarnet siku ya Jumamosi
Naibu rais William Ruto akihutubia wananchi katika eneo la Kabarnet siku ya Jumamosi

Ruto aliongoza ufunguzi wa Kanisa Katoliki la St Joseph Kituro, alizindua maduka katika soko la Kabarnet na kukutana na wakaazi katika mji huo.

Alikuwa mwenyeji wa Gavana wa Baringo Stanley Kiptis, wabunge Joshua Kandie (Baringo Kati), William Cheptumo (Baringo Kaskazini), Charles Kamuren (Baringo Kusini), Daniel Tuitoek (Mogotio), Moses Lesonet (Eldama Ravine) na spika wa bunge la kaunti David Kiplagat.

Pia walikuwepo Gavana wa Turkana Josphat Nanok, wabunge Rigathi Gachagua (Mathira), Caleb Kosotany (Soy), Aisha Jumwa (Malindi), Nixon Korir (Lang'ata), Oscar Sudi (Kapseret), Cornelius Serem (Aldai), Vincent Tuwei ( Mosop), Kimani Ichung'wa (Kikuyu), Gideon Koskei (Chepalungu), Julius Meli (Tinderet), William Kogo (Chesumei), Johana Ng'eno (Emurua Dikirr) na Florence Jematia (EALA).

Maseneta Kipchumba Murkomen (Elgeyo Marakwet), Aron Cheruiyot (Kaunti ya Kericho, Christopher Langat (Bomet) na Mithika Linturi (Meru) pia walihudhuria.

 

Ruto aliwataka wafanyikazi wa umma kuwahudumia Wakenya wote kwa usawa, akisema idara za serikali hazipaswi kutumiwa kuwatisha viongozi fulani.

"Tunapaswa kuacha kutumia polisi kwa sababu za kisiasa. Kenya haifai kuwa na siasa za vitisho na vitisho," Ruto alisema.