Kivumbi! IEBC yaandaa chaguzi ndogo saba

Muhtasari

• Vigogo wa kisiasa nchini, Naibu Rais William Ruto, kiongozi wa ODM Raila Odinga, Musalia Mudavadi wa ANC na Moses Wetang'ula (Ford Kenya) wote wameweka wagombeaji wa vyama vyao.

Kinara wa ANC Musalia Mudavdi na mwenzake wa Ford Kenya Moses Wetang'ula katika eneo la Kabuchai
Kinara wa ANC Musalia Mudavdi na mwenzake wa Ford Kenya Moses Wetang'ula katika eneo la Kabuchai
Image: JOHN NALIANYA

Tume ya uchaguzi nchini IEBC leo inaendesha chaguzi ndogo katika maeneo bunge mawili na wadi tano — uchaguzi ambao wachanganuzi wa kisiasa wametaja kama wa vyama vya kisiasa kupasha misuli moto vikijiandaa kwa Uchaguzi Mkuu wa 2022.

Vigogo wa kisiasa nchini, Naibu Rais William Ruto, kiongozi wa ODM Raila Odinga, Musalia Mudavadi wa ANC na Moses Wetang'ula (Ford Kenya) wote wameweka wagombeaji wa vyama vyao.

Chama tawala cha Jubilee chake Rais Uhuru Kenyatta pia kiko kwenye kinyang’anyiro.

Wapiga kura watachagua wabunge wapya katika maeneo bunge ya Matungu (kaunti ya Kakamega) na Kabuchai (kaunti ya Bungoma).

Watachagua wawakilishi wapya katika wadi ya Huruma huko Uasin Gishu, Hell’s Gate na London huko Nakuru, Kiamokama huko Kisii na Kitise-Kithuku huko Makueni.

Kwa mara ya kwanza, United Democratic Alliance kinachoongozwa na wandani wa naibu rais William Ruto, kimeweka wagombeaji dhidi ya wale wanaodhaminiwa na Chama tawala cha Jubilee.

Huko Kabuchai, upinzani ni kati ya DP Ruto na Seneta wa Bungoma Wetang'ula.

Wanaowania nafasi ya kuwakilisha wananchi wa Kabuchai iliyoachwa wazi kutokana na kifo cha aliyekuwa mbunge Mukwe Lusweti aliyefariki mwaka jana mwezi Desemba ni pamoja na Majimbo Kalasinga (Ford Kenya), Evans Kakai (UDA), Gasper Wafubwa (mgombea huru) na David Kibiti (Green Movement).

Wengine ni Amos Wekesa (Chama cha Shirikisho), Jeremiah Marakkia (UDP) Peter Kapanga (mgombea huru) na Stephen Barasa (MDP).