Raila na Kingi watofautiana kuhusu chama cha wapwani

Muhtasari

• Raila alisema alitekeleza jukumu muhimu katika kumkuza kisiasa Kingi lakini gavana wa Kilifi sasa anataka kumtelekeza wakati anahitaji msaada wake.

Gavana wa Mombasa Hassan Joho, Kinara wa ODM Raila Odinga na gavana wa Kilifi Amason Kingi wakati wa mkutano wa hadhara Mariakani, Kilifi.
Gavana wa Mombasa Hassan Joho, Kinara wa ODM Raila Odinga na gavana wa Kilifi Amason Kingi wakati wa mkutano wa hadhara Mariakani, Kilifi.

Kiongozi wa ODM Raila Odinga alitofautiana vikali na Gavana wa Kilifi Amason Kingi kuhusu msukumo wa baadhi ya viongozi kutoka Pwani kuunda chama cha kisiasa cha eneo hilo.

Wawili hao walikabiliana huko Ganze, Kilifi, wakati wa mkutano wa kuhamasisha umma kuhusu mchakato wa BBI baada ya mambunge sita ya pwani kupitisha Muswada wa marekebisho ya Katiba 2020.

Raila alisema alitekeleza jukumu muhimu katika kumkuza kisiasa Kingi lakini gavana wa Kilifi sasa anataka kumtelekeza wakati anahitaji msaada wake.

 

Kiongozi huyo wa ODM alisema alimsaidia Kingi kushinda uchaguzi wa bunge 2007 baada ya hapo akamfanya waziri katika serikali ya ‘nusu mkate’.

"Nilikuwa naye 2007. Nilimuunga mkono kuwa gavana na sasa wakati wake unamalizika, nilitaka aje kwenye siasa za kitaifa. Sasa anataka kukimbia na anazungumza juu ya Kadu Asili. ODM ilikuwa nzuri kwake kwa muda wote lakini wakati 2022 inakaribia, sasa anasema chama kingine ni bora, "alisema.

Kundi moja la wabunge wa ODM wakiongozwa na Kingi wanashinikiza kuundwa kwa chama cha kisiasa cha pwani.

Vyama ambavyo vina mizizi katika mkoa huo ni pamoja na Kadu Asili, Shirikisho, Republican congress na Umoja Summit.

Kingi alichaguliwa kuwakilisha eneo bunge la Magarini katika Bunge la Kitaifa wakati wa uchaguzi wa 2007. Aliwahi kuwa waziri wa Jumuiya ya Afrika Mashariki na pia aliongoza wizara ya Uvuvi.

Kingi alisema hakukuwa na mipango ya kuunda chama kipya lakini kuimarisha vilivyoko katika mkoa huo ili kupata umoja ambao utaendesha ajenda za kisiasa na kiuchumi za kanda ya pwani.