Rashid Echesa asakwa na polisi kwa madai ya kumpiga afisa wa IEBC

Muhtasari

Afisa huyo  anadaiwa kumzuia mmoja wa mawakala wa UDA kuingia katika ukumbi wa kupigia kura kwa sababu hakuwa na barakoa.

Aliyekuwa waziri wa Michezo Rashid Echesa
Aliyekuwa waziri wa Michezo Rashid Echesa
Image: MERCY MUMO

Aliyekuwa Waziri wa Michezo Rashid Echesa siku ya Alhamisi alinaswa kwenye video akimzaba kofi afisa wa tume ya uchaguzi na mipaka - IEBC katika kituo cha kupigia kura cha Bulonga huko Matungu.

 Duru katika idara ya polisi zasema kwamba maafisa wa polisi wameanzisha msako kumtafuta Echesa kutokana na hatua yake kumshambulia afisa wa IEBC.

 

Kisa hiki kilitokea wakati Echesa akimshutumu afisa wa IEBC Peter Okura kwa kumzuia ajenti wa UDA kushuhudia upigaji kura.

 

"Sheria inasema maajenti wa uchaguzi lazima washuhudie upigaji kura!" alisikika akizungumza kwa sauti ya juu akimwuliza wakala wa IEBC.

Katika video hiyo isiyosikika sana, wakala wa IEBC alijitetea akisema kwamba alikuwa akifuata maagizo.

Lakini kabla hajamaliza kuongea, Echesa alimpiga kofi.

"Uliambiwa na nani? Umeambiwa na nani? Huwezi kuweka maajenti wetu nje. Kwanini unawafukuza nje .... Huu ni upumbavu rafiki yangu ..." Echesa anasema huku akimpiga kofi afisa huyo.

Okura anadaiwa kumzuia mmoja wa mawakala wa United Democratic Alliance kuingia katika ukumbi wa kupigia kura kwa sababu hakuwa na barakoa.

Uchaguzi huo mdogo umevutia wagombeaji 15, miongoni mwao wakiwa wagombea huru, akiwemo mjane wa Murunga Christabel Amunga na mwanawe wa kiume Eugene Ambwere.

Wagombea wengine katika kinyang'anyiro hicho ni Charles Kasamani wa United Democratic Party, Paul Achayo MDG na Faida Auma wa Maendeleo Chap Chap miongoni mwa wengine wengi.