Majimbo Kalasinga wa Ford Kenya anyakua kiti cha Kabuchai

Muhtasari

• Kalasinga alizoa jumla ya kura 19,274 kubwaga wenzake katika uchaguzi huo ambao ulikumbwa na visa kadhaa vya ghasia.

• Kulingana na tawimu za IEBC ni asilimia  51.68 ya watu waliojitokeza kushiriki uchaguzi huo.

Majimbo Kalasinga aonyesha cheti baada ya kutangazwa mshindi wa kiti cha eneo bunge la Kabuchai ameandamana na kinara wa Fork Kenya Moses Wetangula.
Majimbo Kalasinga aonyesha cheti baada ya kutangazwa mshindi wa kiti cha eneo bunge la Kabuchai ameandamana na kinara wa Fork Kenya Moses Wetangula.
Image: John Nalianya

Simiyu Majimbo Kalasinga wa chama cha Ford Kenya ametangazwa mshindi wa uchaguzi mdogo wa kiti cha eneo la Kabuchai.

Kalasinga alizoa jumla ya kura 19,274 kubwaga wenzake katika uchaguzi huo ambao ulikumbwa na visa kadhaa vya ghasia.

Afisa wa IEBC aliyesimamia uchaguzi huo Benson Esuza alimkabidhi Majimbo cheti Ijumaa asubuhi. 

 

Mgombeaji wa chama cha UDA ambaye alikuwa anapigiwa debe na wandani wa naibu rais William Ruto Evans Kaikai alikuwa wa pili kwa kupata kura 6,455. Wengine waliowania kiti hicho ni  Wekesa Amos Wafula wa FPK na kura 1, 454, Waffubwa Gasper Mufutu, mgombeaji huru alipata kura 1,236.

Kulingana na tawimu za IEBC ni asilimia  51.68 ya watu waliojitokeza kushiriki uchaguzi huo.

Katika chaguzi zingine zilizofanyika siku ya Alhamisi, chama cha Wiper kilishinda kiti cha wadi ya Kitise/Kithuki katika kaunti ya Makueni.  Mgombeaji wa Wiper Sebastian Muli Munguti alipata kura 3,892 kumbwaga mpinzani wake wa karibu Joseph Kioko wa chama cha Muungano aliyepata kura 878.

Kioko ambaye alimaliza wa pili alikuwa akipigiwa debe na gavana wa Makueni Kivutha Kibwana.

Kiti hicho kilivutia wagombeaji saba.