Mauaji! Jamaa apokonya polisi bunduki na kuua watu 4 Kisumu

Muhtasari

• Katika tukio hilo, watu wawili akiwemo afisa wa polisi wa trafiki walipata majeraha mabaya.

• Walioshuhudia kisa hicho walisema mshukiwa alikuwa akiwapiga risasi wale ambao walijaribu kumzuia.

Wanachi katika eneo ambapo mshukiwa alikumbana na mauti
Wanachi katika eneo ambapo mshukiwa alikumbana na mauti
Image: MAURICE ALAL

Mwanamume mmoja huko Kisumu siku ya Ijumaa asubuhi alinyakua bastola kutoka kwa afisa wa polisi wa trafiki na kuwaua watu wanne kwa kuwapiga risasi katika kituo cha Mabasi cha Kisumu.

Katika tukio hilo, watu wawili akiwemo afisa wa polisi wa trafiki walipata majeraha mabaya.

Afisa wa trafiki alikimbizwa katika Hospitali ya Aga Khan. Alipigwa risasi tumboni. Mwathiriwa mwingine, mwanamke alipigwa risasi kwenye paja lake.

Mshukiwa alimpiga risasi afisa huyo alipokuwa anajaribu kumfuata kabla ya kupiga risasi manamba mmoja  aliyetajwa kama Kasuku katika kituo cha matatu cha Ahero.

Pia alimpiga risasi kinyozi mmoja kwa jina Daddy mita 20 tu kutoka kwa kituo cha polisi eneo la kuegesha magari.

Walioshuhudia kisa hicho walisema mshukiwa alikuwa akiwapiga risasi wale ambao walijaribu kumzuia.

John Ochieng ambaye ni manamba alisema jamaa alikuwa akiwafyatulia risasi huku akikimbia.

Mwanamume huyo hata hivyo baadaye alizidiwa maarifa na wananchi wenye gadhabu na kuuawa karibu na eneo la Fanana. Alikuwa anajaribu kutoroka kupitia hoteli moja.

Alikuwa amevaa glavu mikononi mwake. Wananchi walisema pia alikuwa amefunika uso wake. Bunduki hiyo imepatikana.

Pia alikuwa na vitambulisho viwili vya kitaifa vyenye majina tofauti.