Mudavadi awika magharibi huku ANC ikinyakua kiti cha Matungu

Muhtasari

• Peter Nabulindo wa ANC alitangazwa mshindi wa uchaguzi mdogo uliokuwa na upinzani mkali baada ya kuzoa jumla ya kura 14, 257 kumpiku David Were wa ODM ambaye alipata kura 10, 565.

Kinara wa ANC Musalia Mudavadi na mbunge mteule wa Matungu Peter Nabulindo
Kinara wa ANC Musalia Mudavadi na mbunge mteule wa Matungu Peter Nabulindo

Kinara wa ANC Musalia Mudavadi alibwaga ODM baada mgombeaji wa chama chake kulambisha sakafu wagombeaji wengine kunyakuwa kiti cha eneo bunge la Matungu kaunti ya Kakamega.

Peter Nabulindo wa ANC alitangazwa mshindi wa uchaguzi mdogo uliokuwa na upinzani mkali baada ya kuzoa jumla ya kura 14, 257 kumpiku David Were wa ODM ambaye alipata kura 10, 565. Alex Lanya wa UDA alikuwa wa tatu kwa kupata kura 5, 513 huku Bernard Wakoli aliyekuwa mgombeaji huru akimaliza wa nne kwa kura 1, 536.

Matokeo yalitangazwa Ijumaa asubuhi na Msimamizi wa Uchaguzi eneo la Matungu John Kirui. Kiti hicho kiliachwa wazi kufuatia kifo cha Justus Murunga Novemba 14 mwaka jana.

 

Wagombea wengine wote isipokuwa mjane wa marehemu Murunga, Christabel Amunga walikuwepo lakini alimtakia Nabulindo heri njema.

Kampeni katika eneo hilo zilikuwa za aina yake huku vigogo wa kisiasa nchini wakitifua vumbi kuona nani ana umaarufu katika kanda ya magharibi.

Mudavadi, Raila na Naibu Rais William Ruto walionekana kutumia chaguzi hizo ndogo kupima umaarufu wao eneo la magharibi huku wote wakijiandaa kwa uchaguzi mkuu mwaka ujao.

Wadadisi wa kisiasa walisema kwamba wakati Mudavadi na mwenzake wa Ford Kenya Moses Wetang'ula walitumia chaguzi ndogo za Matungu na Kabuchai kuthibitisha ushawishi wao kanda ya magharibi, Raila alitumia nafasi hiyo kujaribu kupima ushawishi wake katika mkoa ambao umekuwa nguzo yake kisiasa.

Ruto kwa upande mwingine alikuwa akitumia matokeo ya kura hiyo labda kukuza umaarufu wa UDA hasa baada ya ushindi wa Msambweni ambapo alibwaga ODM kwa kuunga mkono mgombea huru.