NCIC yatoa tahadhari kuhusu ghasia za Alhamisi

Muhtasari

  • Mwenyekiti wa tume hiyo Samuel Kobia anasema wamehuzunishwa kama tume kwamba hata baada ya tahadhari, viongozi wamepuuza na kuendelea kutekeleza maovu.

Mwenyekiti wa NCIC Samuel Kobia
Mwenyekiti wa NCIC Samuel Kobia
Image: Maktaba

Tume ya uiano nchini NCIC imeelezea kutamaushwa na ghasia, vurumai na madai ya kuwahonga wapiga kura katika chaguzi ndogo zilizofanyika siku ya Alhamisi.

Mwenyekiti wa tume hiyo Samuel Kobia anasema wamehuzunishwa kama tume kwamba hata baada ya tahadhari, viongozi wamepuuza na kuendelea kutekeleza maovu.

“Ni jambo la kusikitisha kuona kiongozi akimzaba kofi mtumishi wa umma, sio tu mbele ya umma lakini mbele ya wakenya wote. Hatuwezi kuvumilia hii tena na kama taifa, na tume, lazima tuchukue msimamo,” Kobia alisema.

 

NCIC imesema kwamba itashirikiana kwa karibu na idara zingine za serikali zikiwemo polisi na DCI ili kuwachukulia hatua washukiwa wa ghasia na utovu katika jamii.

Kobia alisisitiza kuwa, walikuwa pia wanashirikiana na mkurugenzi wa mashtaka ya umma DPP kuhakikisha wahalifu waliokamatwa wanafikishwa kortini ili wawe funzo kwa wengine.

NCIC imekariri msimamo kwamba yeyote akakayepatikana na hatia ya kuvuruga amani haruhusiwi kuwania wadhifa wowote mwaka 2022.

Watu kadhaa walijeruhiwa huku wakenya wakitazama kwa mshangao kiwango cha ghasia kilichoshuhudiwa katika chaguzi ndogo zilizoandaliwa siku ya Alhamisi hasa katika maeneo ya Matungu, Kabuchai na eneo la London Kaunti ya Nakuru.

Katika chaguzi hizo aliyekuwa waziri wa michezo Rashid Echesa alionekana kwenye video akimdhulumu afisa wa tume ya uchaguzi IEBC.  Seneta wa Kakamega Cleophas Malala pia anaokena kwenye video moja akimshika matai mwanamume mmoja huku wafuasi wake wakimshambulia mwanaume huyo.

Katika picha moja mwanamume mmoja anoanekana akitembea bila long’i akiwa ameanika makalio yake baada ya kushambuliwa na nguo za kuraruliwa na vijana.

Mara nyingi polisi walilazimika kutumia vitoa machozi kutuliza hali.

 

Katika kisa kingine ilikuwa mguu niponye kwa mbunge wa Lang’ata Nixon Korir baada ya vijana waliokuwa na gadhabu kumuandama na kutaka kumpiga.