Utoaji chanjo ya covid-19 nchini Kenya waanza

Muhtasari

• Zoezi hilo lilizinduliwa rasmi siku ya Ijumaa mwendo wa adhuhuri katika hospitali ya kitaifa ya Kenyatta.

Image: GETTY IMAGES

Ni afueni kwa wahudumu wa afya kote nchini baada ya kuzinduliwa rasmi kwa zoezi la kuwapa chanjo dhidi ya virusi vya corona wahudumu wa afya.

Zoezi hilo lilizinduliwa rasmi siku ya Ijumaa mwendo wa adhuhuri katika hospitali ya kitaifa ya Kenyatta.

Wahudumu wa afya walikuwa wa kwanza kupokea chanjo hiyo ambayo waziri wa Afya Mutahi Kagwe alitaja ni hatua muhimu sana katika vita dhidi ya maambukizi ya virusi vya corona.

Chanjo hiyo tayari imesambazwa katika maeneo yote nchini na kuna hifadhi nane za kuweka chanjo hiyo.

Shehena ya kwanza ya takriban chanjo milioni moja ilitua katika uwanja wa ndege wa kimataifa JKIA usiku wa kuamkia Jumatano na kupokelewa na waziri wa Afya Mutahi Kagwe miongoni mwa viongozi wengine wakuu katika serikali.

"Kwa kweli ni siku njema kwa Kenya. Sasa tuna silaha sawa na bazooka au machine gun katika vita vyetu dhidi ya virusi, "Waziri Kagwe alisema punde tu shehena ya chanjo ya covid-19 ilipotua uwanja wa JKIA.

Chanjo hiyo ya AstraZeneca iliagizwa kutoka taasisi ya Serum ya India.

Serikali ilitangaza kwamba wahudumu wa afya watakuwa wa kwanza kupokea chanjo hiyo ili kupata kikinga ya kutosha dhidi ya virusi hivyo wanapo wahudumia wakenya.

Watu wengine wanaotarajiwa kuwa katika makundi ya kwanza kupokea chanjo hiyo ni walimu, maafisa wa usalama wahudumu wa mahoteli na watu wenye afya duni miongoni mwa makundi mengine yaliyo katika hatari ya kuambukizwa virusi kulingana na kazi zao.

Takriban watu milioni 1.25 wanatarajiwa kupokea njacho hiyo nchini Kenya katika awamu ya kwanza.