Eric Omondi awachiliwa kwa dhamana ya sh. 50,000

Muhtasari

• Mcheshi Eric Omondi aliachiliwa siku ya Ijumaa baada ya kulala korokoroni siku moja.

• Omondi aliachiliwa kwa dhamana ya polisi ya shilingi 50,000 na atafikishwa mahakamani Machi 18.

Maafisa bodi ya filamu wakishirikiana na DCI wamtia mbaroni mcheshi Eric Omondi
Maafisa bodi ya filamu wakishirikiana na DCI wamtia mbaroni mcheshi Eric Omondi

Mcheshi Eric Omondi aliachiliwa siku ya Ijumaa baada ya kulala korokoroni siku moja.

Alishikwa siku ya Alhamisi na anakabiliwa na mashtaka ya kuzalisha na kusambaza filamu bila idhini.

Omondi aliachiliwa kwa dhamana ya polisi ya shilingi 50,000 na atafikishwa mahakamani Machi 18.

 

Alikamatwa na maafisa wa DCI kuhusiana na onyesho lake la “Wife Material” ambalo video zake zimekuwa zikizungushwa mitandaoni na kuibua hisia kali miongoni mwa wananchi.

Bodi ya filamu nchini ilidai kuwa Omondi alikuwa amekwenda kinyume na sheria zinazodhibiti uzalishaji na usambazaji wa filamu nchini Kenya.

Kulingana na taarifa ya bodi ya filamu, Omondi alikiuka sheria zifuatazo;

  1. Hakuna mtu atakayeonyesha filamu yoyote kwenye maonyesho ambayo umma unakubaliwa au kusambaza filamu hiyo isipokuwa amesajiliwa kama mwonyeshaji au msambazaji wa filamu na Bodi filamu na kupewa cheti.
  2. Hakuna filamu au darasa la filamu ambalo litasambazwa, kuonyeshwa, au kutangazwa, hadharani au kwa faragha, isipokuwa kama Bodi imeichunguza na kutoa hati ya idhini.
  3. Mtu yeyote anayeonyesha filamu yoyote kinyume na masharti ya kifungu  (1) au  kifungu (2) atakuwa na hatia.

Bodi hiyo ilisema kwamba itafanya kila juhudi kuambatana na sheria kuzuia uzalishaji na maonyesho ya filamu zisizoruhusiwa kwenye jukwaa lolote linalokusudiwa maonyesho ya umma.

Bodi hiyo imesema kwamba itawalinda watoto kutokana na athari za filamu ambazo ni hatari na hazifai.