Mahakama yakataa ombi la kufuta kesi ya jaribio la mauaji dhidi ya Babu Owino

Muhtasari

• Mahakama mjini Nairobi ilitupilia mbali ombi la DJ Evolve la kutaka itupilie mbali kesi dhidi ya mbunge Babu Owino kwa madai kwamba amemsamehe na anataka kuangazia uponaji wake.

Mbunge wa Embakasi East Babu Owino
Mbunge wa Embakasi East Babu Owino

Mbunge wa Embakasi East Babu Owino siku ya Jumatatu alipata pigo baada ya mahakama kupinga ombi la kutupilia mbali kesi ya jaribio la mauaji dhidi yake.

Mahakama mjini Nairobi ilitupilia mbali ombi la DJ Evolve la kutaka itupilie mbali kesi dhidi ya mbunge Babu Owino kwa madai kwamba amemsamehe na anataka kuangazia uponaji wake.

Hakimu Mkuu Bernard Ochoi amesema kuwa kujiondoa tu mwenyewe sio jambo stahiki katika kesi ambayo mbunge huyo anashitakiwa kwa makosa ya kumpiga risasi Felix Orinda maarufu kama DJ Evolve.

Hakimu mkuu Benard Ochoi Jumatatu amesema kwamba ombi hilo halikufikia mahitajika yanayotakikana ili kesi hiyo iweze kutupiliwa mbali kwa sasa.

Lakini hakimu Ochoi amesema fursa ya majadiliano zaidi bado iko wazi.

Hakimu Ochoi amesema hawezi kutupilia mbali kesi hiyo kwasababu hajui Babu Owino amempa nini DJ Evolve.

"Kujiondoa tu mwenyewe sio sahihi katika hali kama ya kesi hii; wahusika wote wanastahili kujitokeza wazi kuambia mahakama kile ambacho Babu ametoa kwa ajili ya familia," Ochoi amesema.

Mwaka jana mbunge huyo alishtakiwa kwa makosa ya jaribio la kuua kwa kukusudia dhidi ya DJ Evolve katika klabu B.

Aliachiwa huru kwa dhamana.

Iwapo atapatikana na hatia, mbunge huyo anakabiliwa na kifungo cha maisha gerezani.