Raila aanza kujipanga na huenda akaungana na waliokuwa mahasimu

Muhtasari

• Wale walio karibu na Rais wanasemekana kuwa na hamu ya kunadi Muungano wa One Kenya ili kupunguza ushawishi Raila na kumtenga kwenye urithi wa rais Kenyatta 2022.

• Hatua za hivi punde zinatokana na ODM kushindwa katika uchaguzi mdogo wa Matungu ambapo mgombea wake David Were alilambishwa sakafu na Peter Nabulindo wa ANC.

Naibu rais William Ruto na kinara wa ODM Raila Odinga
Naibu rais William Ruto na kinara wa ODM Raila Odinga
Image: MAKTABA

Aliyekuwa Waziri Mkuu na kinara wa ODM Raila Odinga ameanzisha mikakati ya kuunda chombo kipya cha kisiasa kitakasho leta pamoja washirika wapya tayari kwa uchaguzi mkuu wa 2022.

Mikakati ya Raila ilifichuka baada ya waliokuwa washirika wake katika muungano wa NASA kutangaza rasmi siku ya Alhamisi kuhama muungano huo na badala yake kuunda muungano mpya.

Kwa mara ya kwanza, waliokuwa viongozi wenza katika muungano wa NASA Musalia Mudavadi (ANC), Kalonzo Musyoka (Wiper) na Moses Wetangula (Ford Kenya) siku ya Alhamisi walizindua muungano wa ‘One Kenya Alliance’ - kuachana rasmi na ODM.

Muungano wa One Kenya ambao unamjumuisha mwenyekiti wa Kanu Gideon Moi unasemekana kuwa na baraka za wandani wa Rais Uhuru Kenyatta.

Wale walio karibu na Rais wanasemekana kuwa na hamu ya kunadi Muungano wa One Kenya ili kupunguza ushawishi Raila na kumtenga kwenye urithi wa rais Kenyatta 2022.

Kuna mazungumzo pia ya kuwaleta Gavana wa Mombasa Hassan Joho, Amason Kingi wa Kilifi na Salim Mvurya wa Kwale kama sehemu ya mpango wa kumtenga Raila.

Magavana hao watatu siku ya Jumatano walifanya mkutano wa kushtukiza na Uhuru katika Ikulu ya Nairobi, hatua ambayo ilikera kambi ya Raila.

Mkutano huo ulisemekana kumpata Raila na washirika wake kwa mshangao na tayari wanahisi kwamba Uhuru amekuwa akicheza karata chini ya meza ili kupunguza ushawishi wa Raila katika ngome zake.

"Kwa kweli, Jakom hakujulishwa kabla ya mkutano. Alilazimika kumpigia Joho baadaye kuhusu hilo. Lakini walielezea ajenda wakisema ilikuwa juu ya maendeleo ya pwani," afisa mwandamizi wa ODM aliliambia Star kwa sharti la kutotajwa jina.

Joho ni naibu wa Raila katika ODM na nyota yake katika kanda ya Pwani. Ametangaza kuwa atawania urais kwa tikiti ya Chama cha Chungwa, wakati Kingi anapanga kuzindua chama chake.

Hatua za hivi punde zinatokana na ODM kushindwa katika uchaguzi mdogo wa Matungu ambapo mgombea wake David Were alilambishwa sakafu na Peter Nabulindo wa ANC.

Maafisa wa ODM walikuwa wameshutumu 'Deep State; na baadhi ya maafisa katika serikali ya Jubilee kwa kupiga jeki chama cha ANC huko Matungu kwa lengo la kudhoofisha umaarufu wa Raila katika eneo hilo.

Jubilee pia imeamua kuweka mgombea katika uchaguzi mdogo wa Bonchari mnamo Mei 18 licha ya matumaini ya ODM kwamba Uhuru atajiondoa kwenye kinyang'anyiro hicho ili kuunga mkono mgombea wa ODM.

Muungano wa One Kenya siku ya Alhamisi ulitangaza kwamba utamuunga mkono mgombeaji wa Jubilee katika kinyang’anyiro hicho.  Kanu pia ilitangaza kumwondoa mgombea wake na kumuunga mkono Zebedeo Opore wa Jubilee, na kuvuruga matumaini ya Raila kushinda kiti hicho na kuimarisha uungwaji mkono wake katika eneo la Gusii.

"Tumejitoa kwenye uchaguzi na tunataka kuipa Jubilee ushindi wa uhakika huko Bonchari," Gideon Moi, seneta wa Baringo na kinara wa Kanu, alisema.

Muda mfupi tu baada ya muungano wa ‘One Kenya’ kuzinduliwa, ODM ilitangaza kuwa iko tayari kuunda muungano mpya.

"Tukifahamu vyema kuwa ushirikiano ni sehemu muhimu ya siasa zetu, ODM pia inapanga kuunda muungano mpana, bora na wenye ujasiri ambao utatikisa nchi na kubadili siasa za nchi  kwa miaka ijayo," katibu mkuu wa ODM Edwin Sifuna alisema.