Jamaa ahukumiwa miaka 10 kwa kumuua nyanyake kwa sababu ya chakula - Siaya

Muhtasari

• Maxton Omondi alikuwa ameomba mahakama kupunguza hukumu yake kutoka mauji hadi mauaji ya kutokusudia.

• Omondi alikamatwa na kukiri kumuua Akuru na taarifa yake kuandikishwa katika kituo cha polisi.

Image: LAMECK BARASA

Mahakama mjini Siaya imemhukumu jamaa mmoja kifungo cha miaka 10 gerezani kwa kosa la kumuua nyanyake.

Maxton Omondi alikuwa ameomba mahakama kupunguza hukumu yake kutoka mauji hadi mauaji ya kutokusudia.

Kulingana na stakabadhi za mahakama Omondi alikwenda nyumbani kwao eneo la Rarieda  kaunti ya Siaya Februari 8 na kumpata nyanyake Jael Akuru 82, akiwa ameketi kitandani na kutaka ampe chakula.

Jamaa huyo alichukuwa kijiti na kumgonga nyanyake kichwani baada ya marehemu kumwambia kwamba hakuwa na chakula.

Kisha alimvuta nyanyake kutoka kwa kitanda na kumuacha sakafuni akiwa amezirai na kwenda kwa nyumba ya binamuye ambapo alilala.

Siku iliyofuata Akuru alipatikana akiwa amefariki, alikuwa amevuja damu kutoka kichwani. Alikuwa pia amejeruhiwa goti.

Polisi walizuru eneo la tukio na kuuchukuwa mwili na upasuaji wa mwili kufanyika Februari 16 na ikabainika kwamba alifariki kutokana na kuvuja damu sana kwa sababu ya majeraha ya kichwa.

Omondi kisha alikamatwa na kupelekwa katika kituo cha polisi cha Aram. Alikiri kumuua Akuru na taarifa yake kuandikishwa katika kituo cha polisi.

"Ni kweli nilimuua marehemu lakini sikuwa na mpango wa kumuua," Omondi aliwaambia polisi katika kukiri kwake. Mahakamani ombi hilo lilisajiliwa kama "kukana mashtaka".

Mahakamani afisa wa ushauri nasaha Euphemia Kidwoli alitaka mahakama kumfunga Omondi kwa usalama wake mwenyewe.

Alisema jamaa zake walikuwa wameapa kulipiza mauaji ya nyanyake kwa kumuua ikiwa atawachiliwa.

"Jamaa zake upande wa baba yake wana uchungu naye na wako tayari kulipiza kisasi kwa kumuondoa katika ukoo wao iwapo ataonekana hapo. Maana yake ni kwamba mtuhumiwa yuko salama tu mbali na jamii. Hafai kwa adhabu ya nje ya jela, ”aliiambia korti.

Aliambia mahakama kuwa mamake Omondi alifariki mwaka 2003, miaka mitatu baada ya kuzaliwa na akalelewa na wazazi wa mamake.

Alikwenda kuishi na jamaa za upande wa babake mwaka jana Disemba alikuwa akiishi na nyanyake ambaye sasa ni marehemu.

Alikuwa mwanafunzi katika chuo cha kiufundi cha Nyangoma mjini Bondo alikokuwa akifanya kozi ya ufundi wa magari. Wakati wa tukio hilo alikuwa katika mafunzo ya nyanjani.