KCPE: Matokeo kutangazwa katika muda wa wiki mbili

Muhtasari

• Magoha  alisema kwamba zoezi la kusahihisha mitihani hiyo lilikuwa likiendelea vyema huku insha za Kiswahili na Kiingereza zikiwa za pekee zilizosalia.

Waziri wa elimu George Magoha na mtahiniwa wa KCSE
Waziri wa elimu George Magoha na mtahiniwa wa KCSE

Matokeo ya mtihani wa darasa la  nane KCPE yatatolewa katika muda wa wiki mbili zijazo.

Waziri wa Elimu George Magoha siku ya Jumatatu alisema kwamba zoezi la kusahihisha mitihani hiyo lilikuwa likiendelea vyema huku insha za Kiswahili na Kiingereza zikiwa za pekee zilizosalia.

Waziri vile vile alisema kwamba msimizi wa mitihani katika kaunti ya Kitui aliyemfukuza mtahiniwa wakati wa mtihani wa Insha ya kiingereza atakabiliwa kisheria.

Alisema mwanafunzi huyo hata hivyo atapokea matokeo yake na gredi yake itakuwa bila somo alilokosa.

Magoha kwa mara nyingine tena alitoa onyo kali kwa walimu wakuu na maafisa wa elimu kuwa makini zaidi kwa sabababu baadhi yao walikuwa bado ‘wanacheza na karatasi za mtihani’ baada ya kuzichukuwa kutoka kontena.

Alisema ni jambo la kusikitisha kuwa kuna watu wamekuwa wakiwakanganya wanafunzi wanaofanya mtihani.

Alisema hii imekuwa ikifanyika hasa katika karatasi za pili.

"Ninataka kukutahadharisha mapema kuwa kuna wachache kati yetu wanaocheza na karatasi za mitihani baada ya kuzichukua kutoka kwenye kontena za mitihani na ni bahati mbaya," alisema.

Pia alielezea hofu kuhusu kusambazwa kwa karatasi bandia za mitihani na baadhi ya watu na kuwataka wasimamizi wa mitihani kuwa waangalifu zaidi.

"Mnafahamu kusambazwa kwa karatasi bandia na kikundi fulani na watu hawa mnawajua na mnapaswa kuwpuuza," waziri alisema.

Waziri Magoza alikuwa akizungumza baada ya kuongoza zoezi la usambazaji wa mitihani katika kontena ya Kisumu Central.