Rais Suluhu kusuluhisha kizungumkuti cha Corona Tanzania

Muhtasari

• Rais Suluhu kuunda kamati maalum ya wataalam kutathmini hali ya Covid-19 nchini humo. 

• Rais Suluhu alisema kwamba Tanzania lazima iangaliye kwa undani suala hilo na isionekane kuwa ni nchi ya pekee iliyo na msimao tofauti kuhusu janga hili.

Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan
Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan
Image: HISANI

Rais wa Jamhuri ya muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan ametangaza kuunda kamati maalum ya wataalam ili kutathmini hali ya virusi vya Covid-19 nchini humo na kuishauiri serikali yake kuhusu mikakati mahsusi ambayo inafaa kuchukuliwa.

Rais Suluhu ambaye alichukuwa hatamu za uongozi kufuatia kifo cha rais Pombe Magufuli amepata ushabiki na wananchi wengi baada ya kuonekana kulegeza baadhi ya masharti makali ya mtangulizi wake.

Akihutubia maafisa wakuu katika serikali, rais Samia Suluhu alisema kwamba kama taifa Tanzania inafaa pia kuwa na msimamo madhubuti kuhusu janga la Covid-19 ambalo alikiri limeathiri dunia nzima.

 

Alisema kamati maalum atakayoteua itatoa muongozo utakao kuwa nguzo katika sera za kukabiliana na janga la Covid-19 nchini humo.   

“…Waangaliye remedies tunazoambiwa zitatusaidia kwa upana...Halafu watushauri, halifai kulinyamazia, aidha tulikatae au tulikubali bila kufanya tafiti ya kitaalam,” Rais Suluhu alisema.

Marehemu rais Pombe Magufuli alikuwa amepuuzilia mbali kuwepo kwa maambukizi ya virusi vya Covid-19 nchini Tanzania na hata serikali yake ilidinda kuagiza chanjo za covid-19 kama yalivyofanya mataifa mengine.

Rais Suluhu alisema kwamba Tanzania lazima iangaliye kwa undani suala hilo na isionekane kuwa ni nchi ya pekee iliyo na msimao tofauti kuhusu janga hili.

“Tuwe tunasoma mambo ya Covid ulimwengu lakini Tanzania ni desh! desh! desh! lazima tueleweke   hatuwezi kujitenga kama kisiwa, lakini pia lazima tueleweke, rais alisema.