LSK mahakamani kupinga marufuku dhidi ya sekta ya kibinafsi kuagiza chanjo ya Covid

Muhtasari

• LSK inasema uamuzi wa waziri Kagwe kupiga marufuku sekta ya kibinafsi kuingiza na kusambaza chanjo za Covid-19 ni kinyume cha sheria.

Rais wa LSK Nelson Havi
Rais wa LSK Nelson Havi Rais wa LSK Nelson Havi

Chama cha Wanasheria cha Kenya (LSK) kimekwenda mahakamani kupinga uamuzi wa serikali kupiga marufuku uingizwaji wa chanjo za Covid-19 na sekta binafsi.

Katika ombi lililowasilishwa kortini, LSK inasema kuwa uamuzi wa waziri wa wa Afya Mutahi Kagwe kupiga marufuku sekta ya kibinafsi kuingiza na kusambaza chanjo za Covid-19 ni kinyume cha sheria.

"Kupigwa marufuku kwa uingizaji wa chanjo ni changamoto kwa sababu uamuzi kama huo hauwezi kufanywa wakati uwezo wa chanjo ya serikali ni asilimia 30 ya idadi ya watu wa Kenya," LSK ilisema katika ombi lake.

Kupitia Rais wao Nelson Havi, LSK  inataka mahakama izuie utekelezaji wa uamuzi uliofanywa na Kagwe wiki iliyopita kupiga marufuku uingizaji wa chanjo hizo.

Wanataka pia mahakama isitishe uamuzi wa kufutilia mbali leseni za taasisi ambazo zilikuwa zikiingiza na kutoa chanjo hiyo kwa umma.

LSK pia inataka kutupiliwa mbali kwa agizo la kufungwa kwa nchi lililotolewa na Rais Uhuru Kenyatta mnamo Machi 26 ikisema agizo linakiuka sheria.