Mama wa kambo wa Barack Obama afariki siku chache baada ya nyanyake kuaga

Muhtasari

• Keziah Onyango alifariki Jumanne jioni nchini Uingereza; binti yake Auma Obama alithibitisha.

Mama wa kambo wa rais mustaafu wa Marekani Barack Obama, Keziah Onyango alifariki Jumanne usiku
Mama wa kambo wa rais mustaafu wa Marekani Barack Obama, Keziah Onyango alifariki Jumanne usiku
Image: MAKTABA

Mama wa kambo wa Rais mstaafu wa Amerika Barack Obama ameaga dunia.

Keziah Onyango alifariki Jumanne jioni nchini Uingereza; binti yake Auma Obama alithibitisha.

"Nilimpoteza mamangu mpendwa jana. Nimeganda," Auma Obama aliandika tweet siku ya Jumatano asubuhi.

 

Keziah 81, amekuwa akiugua kwa muda mrefu.

Bado haijulikani kama marehemu atazikwa baadaye Jumatano, Aprili 14 nchini Uingereza kuambatana na tamaduni za dini ya Kiislamu.

Wiki mbili zilizopita, familia ya Obama ilimzika Mama Sarah Onyango Obama nyumbani kwake Kogelo katika hafla ya kibinafsi iliyohudhuriwa na familia yake, maafisa wakuu wa serikali, jamaa na marafiki.

Hafla fupi ya mazishi ambayo ilifanywa kulingana na tamaduni za Kiislamu ilifuata ibada fupi ya mazishi ambayo iliongozwa na Sheikh Musa Ismail muda mfupi baada ya saa sita mchana.

Wanawake hawakuruhusiwa kuingia makaburini kulingana na kanuni za Kiislamu.

Alizikwa karibu na mumewe Hussain Onyango.

Waziri wa Maswala ya Kigeni Raychelle Omamo aliwaongoza maafisa wa serikali na viongozi wengine kutoa heshima zao za mwisho kwa Mama Sarah.