Martha Koome ajitosa mbele ya JSC akisaka wadhifa wa Jaji Mkuu

Muhtasari

• Kuhusu majaji 41 ambao rais Uhuru Kenyatta alidinda kuteua, Koome alisema atazungumza na rais kuwateua.

Jaji wa mahakama ya rufaa Martha Koome alipofika mbele ya JSC kuhojiwa kuhusu wadhifa wa jaji mkuu, 14/04/2021.
Jaji wa mahakama ya rufaa Martha Koome alipofika mbele ya JSC kuhojiwa kuhusu wadhifa wa jaji mkuu, 14/04/2021.
Image: CHARLENE MALWA

Jaji wa mahakama ya rufaa Martha Koome kwa mara nyingine tena anajaribu bahati kusaka nafasi ya kuongoza idara ya mahakama nchini.

Koome leo Jumatano amefika mbele ya tume ya huduma kwa mahakama (JSC) kupigwa msasa na kunadi sera zake ikiwa atateuliwa kuwa rais wa mahakama ya upeo.

Koome katika taarifa yake ya utangulizi alisema kwamba ikiwa atapata fursa ya kuongoza idara ya mahakama atahakikisha anatakeleza operesheni za hazina ya idara ya mahakama ili kukabili changamoto za kila wakati za uhaba wa fedha katika idara hiyo.

 

Alibainisha kuwa kwa sasa kuna miradi mingi ambayo imesimama kwa sababu ya ukosefu wa fedha na hii pamoja na mambo mengine itatatuliwa.

Jaji Koome pia alisema ataweka mfumo ambao utafuatilia thamani ya pesa.

Kuhusu majaji 41 ambao rais Uhuru Kenyatta alidinda kuteua, Koome alisema atazungumza na rais kuwateua.

Ili kuwahudumia Wakenya vizuri, alisema, ataweka njia za kisasa za mawasiliano kama vile matumizi ya arafa kuwezesha wahusika kujua maendeleo ya kesi zao.

Jaji Koome alizaliwa katika familia ya wakulima katika kijiji cha Kithiu eneo la Miragamieru huko Meru lakini alikabili changamoto hizo zote na sasa anatambuliwa kimataifa kama mtetezi wa haki za binadamu na jaji wa mahakama ya rufaa.

Ana uzoefu wa miaka 33 katika taaluma ya sheria, huku muda wake mwingi  akiwa katika utumishi wa umma kama mtetezi wa haki za binadamu.

Kwa hili amepata sifa za kimataifa kwa mchango mkubwa kwa sheria katika upanuzi wa Utawala wa sheria na ulinzi wa wanyonge.

 

Yeye ni mwanasheria wa maswala ya familia na huegemea sana haki za watoto kazi ambayo ilifanya  atambuliwe na Umoja wa Mataifa ambapo alichaguliwa kama mtu mashuhuri wa Umoja wa Mataifa wa mwaka 2020.