MCA 2 wakamatwa kuhusiana na ghasia katika bunge la Nyamira

Muhtasari

• MCA wa Magwagwa Fred Omayio na mwenzake wa Kiabonyoru Duke Omoti wanadaiwa kushambuliwa na maafisa wa usalama ambao walikuwa wamevaa nguo za raia.

Image: ALVIN RATEMO

Wakilishi wadi wawili wa Bunge la kaunti ya Nyamira siku ya Alhamisi walikamatwa ndani ya ukumbi wa mijadala baada ya vurumai kuzuka bungeni humo kwa mara ya tatu mfululizo.

MCA wa Magwagwa Fred Omayio na mwenzake wa Kiabonyoru Duke Omoti wanadaiwa kushambuliwa na maafisa wa usalama ambao walikuwa wamevaa nguo za raia.

Wawili hao walitolewa nje ya bunge wakiwa wamewekwa pingu. Shughuli za bunge zilisitishwa kwa muda wa dakika thelathini.

Shida ilianza wakati spika Moffat Teya aliamuru MCA, Laban Masira (Nyamaiya), Duke Omoti (Kiabonyoru) na Fred Moayio (Magwagwa) ambao walikuwa wanatumikia marufuku ya muda kuondoka kwenye ukumbi wa mijadala.

Image: ALVIN RATEMO

Walidinda kuondoka na kulazimisha maafisa wa usalama kutumia nguvu lakini juhudi zao zilikwamishwa na wakilishi wadi wengine waliosema kufurushwa kwao kulikuwa kinyume cha sheria.

Ili kukinga wenzao, wakilishi wadi walishirikiana kuwashambulia maafisa wa usalama.

Baada ya wawakilishi wadi hao watatu kuondolewa nje ya bunge wakilishi wadi waliosalia walibaki wakiimba na kumrushia maneno makali spika wa kaunti.

Spika alisisitiza kwamba hangeweza kuruhusu utovu wa nidhamu katika ukumbi wa mjadala.