Mgogoro wa chini kwa chini kati ya Iran na Israel umefika hatua hatari

Muhtasari

• Iran imelaumu Israel kwa mlipuko uliotokea na kuathiri kiwanda cha utengenezaji madini ya urani katika mtambo wa Natanz.

Mtambo wa Natanz umelindwa vikali, ukiwa na mashinechini ya ardhi
Mtambo wa Natanz umelindwa vikali, ukiwa na mashinechini ya ardhi
Image: EPA

Mzozo wa muda mrefu kati ya nchi mbili za Mashariki ya Kati, Iran na Israel, unaonekana kuendelea kutokota.

Iran imelaumu Israel kwa mlipuko uliotokea na kuathiri kiwanda cha utengenezaji madini ya urani katika mtambo wa Natanz.

Israel haijasema hadharani ikiwa ndio iliyotekeleza shambulizi hilo ambalo Iran inasema ni "kitendo cha hujma" lakini vyombo vya habari vya Marekani na Israel vimenukuu maafisa waliosema kikosi cha kijasusi cha Israel nje ya nchi, Mossad ndicho kilichotekeleza shambulizi hilo.

Kwa upande wake, Iran imeapa kulipiza kisasi.

Lakini hili sio tukio pekee linaloweza kuangaziwa. Kumekuwa na mashambulizi ya kulipizana kisasi kutoka kwa pande zote mbili huku zikionesha kuwa makini kutoingia katika mgogoro wa moja kwa moja ambao uthaathiri pakubwa nchi zote mbili.

Baada ya tangulizi hiyo, je hatari zilizopo ni gani na mzozo huo unaweza kuisha vipi?

Vita hivyo vya chini kwa chini vinaweza kugawanywa katika sehemu tatu.

Mpango wa nyuklia wa Iran

Israel haiamini kuwa mpango wa nyuklia wa Iran ni wa amani badala yake inaamini kwamba Iran inaendeleza mpango wa kutengeneza vichwa vya makombora ya nyuklia kisiri na namna ya kuvisafirisha kwa kutumia makombora.

Akizungumza Jumatatu, wakati wa ziara ya Waziri wa Ulinzi wa Marekani Lloyd Austin, Waziri Mkuu wa Israel Benyamin Netanyahu alisema: "Mashariki ya kati kuna tishio moja ambalo liko katika hatua mbaya, hatari mno, ambalo ni nyeti zaidi hata kuliko lililowekwa na utawala wenye msimamo mkali nchini Iran.

Pia Jumatatu, balozi wa Israel huko London, Tzipi Hotovely, alielezea BBC kuwa: "Iran haijawahi kuacha kuendeleza mpango wake wa silaha za nyuklia na makombora. Uendelezaji wa silaha za nyuklia na Iran... ni tishio kwa dunia nzima."

Israel ikiendelea kuwa na fikra hizo, imekuwa ikichukua mfululizo wa hatua za pande moja na hata zingine ambazo hata hawazitangazi hadharani kujaribu kupunguza kasi au kulemaza mpango wa nyuklia wa Iran.

Hii ikiwa ni pamoja na kutumia virusi vya kompyuta vilivyogunduliwa kwa mara ya kwanza mwaka 2010 na kuharibu mashine za Iran. Awali karne hii, idadi kadhaa ya wanasayansi wa Iran walifariki dunia kwa njia isiyoeleweka na Novemba 2020 kukatokea mauaji ya mtu wa ngazi ya juu wa Iran karibu na Tehran Mohsen Fakhrizadeh.

Hakuwa tu kiongozi mkuu wa timu ya wataalamu wa nyuklia lakini pia alikuwa anashikilia nafasi ya juu katika kikosi maalum cha jeshi nchini humo na Israel inaamini kuwa yeye ndio alikuwa akiendesha mpango wa nyuklia wa Iran.

Sasa hivi Rais wa Marekani Joe Biden anajitahidi kurejesha tena nchi hiyo katika makubaliano ya kihistoria ya mpango wa nyuklia wa Iran yaliyofikiwa mwaka 2015 lakini baadaye, aliyekuwa Rais Donald Trump akajitoa kwenye makubaliano hayo na kama haitoshi akaiwekea tena Iran vikwazo vya kiuchumi.

Hata hivyo kuna changamoto kwasababu Iran imeonesha kutokuwa tayari kuunga mkono hatua ya Biden kwa kusema: ''Hapana, hatuwaamini tena na sasa ikiwa hiyo ndio nia yenu, itabidi nyinyi mujitokeze kwanza. Tutatimiza kikamilifu makubaliano punde tu vikwazo kiiondolewa''.

Na ili kujaribu kukabiliana na mkwamo huo, wapatanishi kutoka nchi kadhaa wanakutana huko Vienna. Lakini bado Israel haiamini kuwa kuna umuhimu wa kufufua mazungumzo ya nyuklia ya Iran.

"Israel kwa juhudi zake za pande moja inajaribu kuvuruga mpango wa nyuklia wa Iran, kwa kusambaratisha uwezo wake wa kiufundi hatua ambayo imegeuka kuwa mchezo hatari.

Kwanza juhudi hizi za Israel zinaweza kusambaratisha mazungumzo na Marekani wakati ambapo inataka kurejea tena katika makubaliano.

"Lakini pili, Iran inaweza kuamua kulipiza kisasi kwa kufanya mashambulizi dhidi ya Israel na kulenga washirika wake kote duniani. Israel imethibitisha kuwa inaweza kuvuruga mpango wa Iran lakini swali ni je kwa gharama gani? "

Safari za majini

Matukio ya ajabu ajabu yamekuwa yakitokea baharini siku za hivi karibuni. Mapema mwaka huu, meli ya kubeba mizigo ya Israel, MV Helios, iliharibiwa vibaya wakati inapita kwenye ghuba ya Oman.

Ilitobolewa mashimo mawili kwa chini na Israel inalaumu Iran. Hata hivyo, iran imekanusha kuhusika na kitendo hicho.

Aprili, meli Saviz, meli ya Iran iliyokuwa imetia nanga kusini mwa Bahari ya Shamu, pia nayo ilitobolewa kwa chini. Israel na muungano unaoongozwa na Saudia karibu na Yemen wanaamini kuwa meli hiyo imekuwa ikitumika na kundi la wanamgambo wa Houthi ambao ni washirika wa Iran waliopo nchini Yemen.

Vyombo vya habari vya Marekani vimesema kuwa katika kipindi cha miezi 18 iliyopita, vikosi vya Israel vimelenga karibu meli 12 zilizokuwa zinaelekea Syria ambazo zilikuwa zimebeba mafuta ya Iran na vifaa vya kijeshi.

Syria na Lebanon

Ukweli wa kwamba Syria imekuwa vitani katika kipindi cha miaka 10 iliyopita, hilo limekuwa angalizo kubwa duniani huku vitendo vinavyotekelezwa na Israel vikifumbiwa jicho.

Vita vya wenyewe kwa wenyewe vimetoa mwaya na kuruhusu Iran kushirikiana na washirika wake waliopo Lebanon, Hezbollah, kuunga mkono utawala wa Rais wa Syria Bashar al- Assad.

Eneo la Golan Heights lililotwaliwa na Israeli liko katika maeneo yanayolengwa na vikosi vya Iran
Eneo la Golan Heights lililotwaliwa na Israeli liko katika maeneo yanayolengwa na vikosi vya Iran
Image: GETTY IMAGES

Hitimisho

Pande zote mbili hazitaki kuonekana kuwa ni dhaifu lakini Iran na Israel zinafahamu fika umuhimu wa kuwa makini mno na matendo yao ili zisiwe chachu ya vita.

Upande wa nyuklia ni wazi kuwa ujasusi wa Israel umefanikiwa kupenya hadi kwenye usalama wa Iran kwa kiasi kikubwa, kwa maana ya kuwa na maajenti wao binafsi wanaofuatilia taarifa moja kwa moja na uvamizi wa silaha kukabiliana na Iran.

Mwaka 2018, waziri mkuu wa Israeli Benjamin Netanyahu alifichua kile alichodai ni makavazi ya siri ya Iran ya atomiki
Mwaka 2018, waziri mkuu wa Israeli Benjamin Netanyahu alifichua kile alichodai ni makavazi ya siri ya Iran ya atomiki

Kwa Syria na Lebanon huwa kuna chaguo kwa Iran kupeleka wawakilishi wake kufanya mashambulizi ya anga dhidi ya Israel lakini hatua hii ni hatari zaidi.

Israel imesema wazi vile itakavyojibu hatua kama hiyo hadi kiasi itakavyopenyeza nchini Iran.