Uhuru akubali shinikizo za wakenya azuia kupandishwa kwa bei za mafuta

Muhtasari

• Hii ni licha ya gharama ya petroli kutoka nje kuongezeka kwa asilimia 9.27 hadi $ 4491.50 kwa kila mita moja mraba ikilinganishwa na $ 449.82 mwezi Februari.

Mhudumu akiweka gari Mafuta ya petroli
Mhudumu akiweka gari Mafuta ya petroli
Image: MAKTABA

Hatua ya dakika za mwisho ya wizara ya fedha ililazimisha mamlaka ya kudhibithi kawi nchini kutopandisha bei za mafuta ya petroli baada ya wakenya kulalamikia uwezekano wa kupanda kwa bei hizo.

Barua kutoka kwa wizara hiyo kwa kaimu mkurugenzi wa mamlaka ya EPRA Daniel Kiptoo ilionyesha kuwa serikali itawalipa fidia wauzaji wa mafuta.

"Kwa hivyo lengo la barua hii ni kuidhinisha EPRA kuchapisha bei za mafuta kwa kipindi cha Machi 15 hadi Aprili 14 kuendelea kutumika katika kipindi cha moja cha Aprili 15 hadi Mei 14," sehemu ya barua hiyo ilisema.

Siku ya Jumatano, vyombo vya habari nchini Kenya ikiwemo Radio Jambo vilionya kuhusu ongezeko la bei ya mafuta na kuibua mjadala mkali miongoni mwa wakenya.

"Bei ya petroli, dizeli na mafuta ya taa kusalia bila kubadilika kwa mwezi mmoja ujao hadi Mei 14 wakati bei mpya zitatolewa," EPRA ilisema bila kutoa sababu ya kubakiza bei za rejareja.

Lita moja ya petroli itaendelea kuuzwa kwa Shilingi 122.81 jijini Nairobi, dizeli 107.66 na lita moja ya mafuta ya taa kuuza kwa Shilingi 97.85 kwa mwezi mmoja hadi Mei 14.

Hii ni licha ya gharama ya petroli kutoka nje kuongezeka kwa asilimia 9.27 hadi $ 4491.50 kwa kila mita moja mraba ikilinganishwa na $ 449.82 mwezi Februari. Mita moja mraba ya ya dizeli na mafuta ya taa pia iliongezeka kwa asilimia 4.77 na 7.29 mtawaliwa.

Wataalamu wa uchumi walikuwa wameonya kuhusu hali ngumu ya maisha kwa wananchi wengi ambao tayari wanakabiliwa na changamoto zinazotokana na athari za Covid-19 endapo serikali ya Rais Uhuru Kenyatta ingeongeza tena bei ya mafuta.