Uhuru aomboleza kifo cha aliyekuwa mkuu wa mkoa John Etemesi

Muhtasari

 • John Etemesi alihudumu katika nafasi ya Naibu mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Pwani na baadaye kama mkuu wa Mkoa, Mashariki na baadaye Mkoa wa Kati.

Aliyekuwa mkuu wa mkoa John Khabeko Etemesi.
Aliyekuwa mkuu wa mkoa John Khabeko Etemesi.
Image: HISANI

Rais Uhuru Kenyatta ametuma ujumbe wa risala za rambi rambi kwa familia na marafiki wa aliyekuwa mkuu wa Mkoa John Khabeko Etemesi.

Etemesi alifariki asubuhi ya Aprili 26 nyumbani kwake Sibanga huko Cherengany, Kaunti ya Trans Nzoia.

Alikufa akiwa na umri wa miaka 90 na aliwahi kuwa mkuu wa mkoa wakati wa enzi ya Marehemu Rais Daniel arap Moi.

Katika ujumbe wake wa kutia moyo na faraja, Rais alimuelezea marehemu Etemesi kama Mkenya mwaminifu na mzalendo aliyeitumikia nchi kwa kujitolea sana.

"Mzee John Etemesi alikuwa mtu mnyenyekevu, mtumishi wa umma mwenye bidii na mchapakazi ambaye aliacha alama isiyofutika katika mikoa yote ya nchi yetu ambapo aliwekwa kutumikia," Uhuru alisema.

"Mzee Etemesi alikuwa msimamizi mzuri sana ambaye alifundisha watu wengi katika utumishi wa umma kuwa viongozi bora na watumishi."

John Etemesi alihudumu katika nafasi ya Naibu mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Pwani na baadaye kama mkuu wa Mkoa, Mashariki na baadaye Mkoa wa Kati.

Baada ya kustaafu kutoka kwa Utawala wa Mkoa, marehemu aliendelea kutumikia bodi kadhaa za mashirika ya serikali na Tume.