Hospitali ya Kenyatta kuhudumia wagonjwa wa dharura pekee

Muhtasari

• Mkurugenzi mkuu wa NMS Mohammed Badi siku ya Jumatano alisema kikosi chake pamoja na Wizara ya Afya wamefanyia mabadiliko mfumo wa rufaa.

• Hii inamaanisha kwamba hospitali zote za kiwango cha 3, 4 na 5 ndani ya Nairobi zitashughulikia wagonjwa wa matatizo madogo madogo.

Mkurugenzi wa NMS Meja jenerali Mohamed Badi
Mkurugenzi wa NMS Meja jenerali Mohamed Badi

Hospitali ya Kitaifa ya Kenyatta kuanzia Julai itaanza kushughulikia rufaa tu wakati inafunga milango kwa wagonjwa wanaotembea.

Mkurugenzi mkuu wa NMS Mohammed Badi siku ya Jumatano alisema kikosi chake pamoja na Wizara ya Afya wamefanyia mabadiliko mfumo wa rufaa.

"Ili kutekeleza mpango huu na Nairobi kuwa ya kwanza kufanyiwa majaribio, kuanzia Julai, KNH itafunga milango yake kwa wagonjwa wasiohitaji huduma za dharura," alisema.

Hii inamaanisha kwamba hospitali zote za kiwango cha 3, 4 na 5 ndani ya Nairobi zitashughulikia wagonjwa wa matatizo madogo madogo.

Badi alisema kuwa kwa kushirikiana na Kaimu Gavana Anne Kananu, juhudi zote zitafanywa kuhakikisha hospitali 24 zilizoahidiwa na Rais Uhuru Kenyatta zinafanya kazi kikamilifu.

Uhuru alikuwa amesema awali kuwa ujenzi wa hospitali 24 ulithibitisha kuwa maendeleo yanaweza kupatikana mahali popote Nairobi kwa kutumia pesa kidogo sana.

badi
badi

“Umma sasa unaweza kupata huduma za afya bila kulazimika kusafiri hadi KNH. Ninajivunia kazi nzuri mkurugenzi mkuu wa NMS Meja jenerali Mohamed Badi na timu yake wamefanya katika kujenga vifaa hivi katika maeneo ya mbali ndani ya Nairobi, "alisema.

Mwaka wa 2016, waziri wa afya wakati huo Cleopa Mailu alikuwa ametangaza mipango ya KNH kukoma kutoa huduma za wagonjwa wa nje ikiwa hospitali za kaunti zitaboresha huduma zao.

“Tunataka kuimarisha huduma zinazotolewa katika hospitali. Tunakusudia pia kujumuisha huduma za wagonjwa wa ndani katika hospitali hizo, na hivyo kuunda nafasi ya kushughulikiwa kwa visa vya rufaa katika KNH, ”alisema.

Mipango hiyo sasa inahakikiwa baada ya Rais mwaka jana kuagiza Badi kujenga vituo 24 vya afya kwa gharama ya Shilingi bilioni mbili.

Hospitali za nyongeza zilipaswa kupunguzia mzigo hospitali za KNH, Mama Lucy, Pumwani na Mbagathi.

NMS ilipewa jukumu la kujenga vituo vya afya 19 kila moja kwa Shilingi milioni 70 na tano zitakarabatiwa kwa Shilingi milioni 300.

Kumi kati ya vituo vipya ni hospitali za kiwango cha 2 wakati zingine ni kiwango cha 3.

Rais Uhuru tayari ameagiza hospitali nne kati ya 24: Hospitali ya Uthiru-Muthua ni kiwango cha 3 wakati zingine tatu - Kiamaiko, Soweto na Ushirika - ni vituo vya kiwango cha 2.

Tayari NMS imeajiri wafanyikazi wa huduma ya afya 2,000 kati yao wataalam 44, wauguzi 679, madaktari 130 kuhakikisha kuwa wahudumu sio kikwazo kwa utoaji wa huduma bora katika hospitali zote mpya 24 na vituo vingine.