Mahakama kuamua hatma ya mchakato wa BBI leo alasiri

Muhtasari

• Jopo la majaji Joel Ngugi, George Odunga, Jarius Ngaah, Janet Mulwa na Chacha Mwita wamepangiwa kutoa uamuzi wao kuhusu maombi saba yanayopinga mchakato wa BBI.

• Muswada wa marekebisho ya katiba maarufu  tayari umeidhinishwa na bunge la kitaifa na seneti na unatarajiwa kuwasilishwa kwa rais Uhuru Kenyatta atakaye ukabidhi kwa IEBC ili kura ya maamuzi iandaliwe.

Mahakama hivi leo alasiri inatarajiwa kutoa uamuzi ambao utatoa mwelekeo kuhusu mchakato wa marekebisho ya katiba kuambatana na mwafaka wa BBI.

Jopo la majaji Joel Ngugi, George Odunga, Jarius Ngaah, Janet Mulwa na Chacha Mwita wamepangiwa kutoa uamuzi wao kuhusu maombi saba yanayopinga mchakato wa BBI.

Mnamo Februari, BBI ilipata pigo kubwa baada ya Mahakama Kuu kuizuia IEBC kuanzisha mipango ya kura ya maamuzi kuhusu Muswada wa marekebisho katiba, 2020.

Katika uamuzi uliotolewa na jopo la majaji watano, Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) ilisimamishwa kwa muda kujiandaa kwa kura ya maamuzi na inasubiri kusikilizwa na kuamuliwa kwa maombi saba yaliyowasilishwa kupinga mchakato huo. 

Majaji walikuwa wameonya zaidi Bunge na mabunge ya kaunti dhidi ya kuharakisha mchakato wa BBI.

"Kukimbiza Muswada kupitia mikutano ya kaunti na mwishowe kupitia Bunge hakuingizi mabadiliko ya katiba yanayotokana na uwezekano kwamba inaweza kutangazwa kuwa batili," majaji waliamua.

Muswada wa marekebisho ya katiba maarufu BBI tayari umeidhinishwa na bunge la kitaifa na seneti na unatarajiwa kuwasilishwa kwa rais Uhuru Kenyatta atakaye ukabidhi kwa IEBC ili kura ya maamuzi iandaliwe.