Afisa wa DCI mahakamani kwa madai ya mauaji Embakasi

Muhtasari

• Afisa huyo wa inasemekana siku ya Alhamisi asubuhi alikuwa amezozana na mlinzi wa usiku kabla ya kumuua mlinzi huyo kwa kumpiga risasi.

• Alimpiga risasi jamaa huyo Lapaja Topiwo, 23 mara mbili kifuani.

Crime scene
Crime scene

Afisa mkuu wa DCI wa Embakasi-Nairobi Simon Mutia Mwongela atarajiwa kufikishwa mahakamani leo Jumatatu kutokana na kisa na ufyatulianaji risaji mtaani Embakasi.

Mwongela alilazimika kulala korokoroni wikendi yote kufuatia tukio la kupigwa risasi kwa mlinzi wa usiku huko Kayole, Nairobi.

Afisa huyo mwenye cheo cha SSP huenda akasalia korokoroni kwa siku zaidi kwani maafisa wanaochunguza tukio hilo wanatarajiwa kuomba mahakama kwa muda zaidi ili kuwawezesha kumamilisha uchunguzi kuhusu mashtaka ya mauaji dhidi ya afisa huyo wa DCI.

Mwongela alikuwa amezuiliwa kwenye seli za polisi za Kileleshwa wikendi yote kwa sababu Ijumaa ilikuwa siku kuu ya Idd Fitr.

Afisa huyo wa polisi inasemekana kwamba siku ya Alhamisi asubuhi alikuwa amezozana na mlinzi wa usiku katika Hoteli ya Night Square mtaani Embakasi na kabla ya kumuua mlinzi huyo kwa kumpiga risasi.

Alimpiga risasi jamaa huyo Lapaja Topiwo, 23 mara mbili kifuani.

Mashahidi waliambia polisi kuwa Mwongela alikuwa ameletwa kwenye hoteli hiyo saa nane usiku Mei 14 na kulala kidogo kwa takriban saa mbili kabla ya kuamka na kuleta vurugu.  Baadaye alinyang'anywa silaha na kukamatwa baada ya tukio hilo.