SIKU YA KUADHIMISHA BARA AFRIKA

Raila asihi Waafrika kuboresha Afrika badala ya kwenda ng'ambo

Amewataka Waafrika kutafakari vita chungu ambazo zilipiganwa na mababu kujikomboa toka mikononi mwa wakoloni ili waweze kukataa matendo ya kurudisha bara kwenye siku za ukoloni.

Muhtasari

•Amewataka Waafrika kutafakari vita chungu ambazo zilipiganwa na mababu kujikomboa toka mikononi mwa wakoloni ili waweze kukataa matendo ya kurudisha bara kwenye siku za ukoloni.

•Pia amehimiza nchi za Kiafrika kuwashikilia vijana ili watimize uwezo wao huku akisema kuwa wao ndio rasilimali kubwa sana.

Raila Odinga
Raila Odinga

Kinara wa ODM Raila Odinga amewataka Waafrika kutumia mawazo na nguvu zao kuboresha bara Afrika. Amewaagiza Waafrika kuepuka juhudi zozote za kurudisha bara Afrika nyuma kwenye siku za ukoloni.

Akitoa ujumbe wa kuadhimisha siku ya bara Afrika Jumanne, Raila ametaja kuwa siku za kikoloni Afrika ilisaidia nchi nyingi ulimwenguni  kuendelea na kusema kuwa wakati wa Waafrika kuendeleza bara lao umefika.

Amewataka Waafrika kutafakari  vita chungu ambazo zilipiganwa na mababu ili kujikomboa toka mikononi mwa wakoloni waweze kukataa matendo yoyote ya kurudisha bara kwenye siku za ukoloni.

‘’Miaka iliyopita, mababu zetu walilazimishwa kupita kwenye milango ambayo huwezi rudi nyuma ili waende wakawe watumwa katika nchi za mbali, ni kinaya kuwa sasa watu wanajitakia kupitia milango hiyo kufika nchi zile wakitafuta kazi” Raila alisema huku akisisistiza kuwa yafaa Waafrika waone haya kutokana na jambo hilo.

Raila amehimiza nchi za Kiafrika kuwashikilia vijana ili watimize uwezo wao huku akisema kuwa wao ndio rasilimali kubwa sana.

Waafrika nawasihi tusitishwe na lolote. Lazima tudai kuthamini kwa utu na kuheshimiwa. Nasi lazima tuonyeshe heshima ili tuheshimiwe pia” Raila alisema