SIKU YA MAOMBI NCHINI

Ruto asifu uongozi wa Rais Kenyatta katika vita dhidi ya Korona

Naibu rais pia alimpongeza spika wa bunge la kitaifa, Justin Muturi kwa kutawazwa kuwa msemaji wa eneo la Mlima Kenya

Muhtasari

•Ruto alisherehekea kuteuliwa kwa Martha Koome kama  Jaji mkuu mwanamke wa kwanza na kumpongeza kwa uteuzi huo

•Naibu rais pia alimpongeza spika wa bunge la kitaifa, Justin Muturi kwa kutawazwa kuwa msemaji wa eneo la Mlima Kenya.

Naibu Rais William Ruto
Naibu Rais William Ruto
Image: Hisani

Naibu rais William Ruto amempongeza uongozi wa Rais Uhuru Kenyatta katika vita dhidi ya virusi vya Korona na miradi aliyozindua.

Akiongea katika  ibada ya maombi ya taifa, Ruto ameangazia dunia yote ilivyoathiriwa na janga la Korona. Ruto hata hivyo amepongeza juhudi za Rais Kenyatta kudhibiti hali nchini.

Mambo yaliharibika sana, lakini mtukufu rais kwa sababu ya uongozi wako hali nchini iliimarishwa na tukaweza kujiinua tena. Wizara ya afya imefanya kazi nzuri na sasa tunazungumza  tutakavyopatia watu chanjo ili tuweze kujitoa kwenye janga hili na tuweze kusuluhisha shida za kiuchumi na zinginezo” Ruto alisema.

Ruto ambaye imekadiriwa kwa muda sasa kuwa hajakuwa katika hali ya maelewano na Rais tangu salamu za Handshake kati yake na aliyekuwa waziri mkuu, Raila Odinga, pia alimsifu rais kwa kuzindua bandari ya Lamu kati ya miradi ingine ambayo rais amezindua.

Kwenye hotuba yake, Ruto alisherehekea kuteuliwa kwa Martha Koome kama  Jaji mkuu mwanamke wa kwanza na kumpongeza kwa uteuzi huo. Pia alimpongeza spika wa bunge la kitaifa, Justin Muturi kwa kutawazwa kuwa msemaji wa eneo la Mlima Kenya.

Naibu rais pia alisisitiza kuwa wakati umefika wa viongozi kufanya kazi pamoja huku akisema kuwa kusimama kwa ziara za tangatanga na kutupiliwa mbali kwa mchakato wa BBI kuwa ni ishara kuwa Mungu anawataka viongozi kuwaza pamoja.

Kwa sasa ziara za Tangatanga zimesimama, na reggae pia imesimama. Nadhani yafaa tuskize maneno ya askofu aliyetusihi kufanya kazi pamoja, tufanye kitu pamoja” Ruto alisema.