UTEUZI WA MAKAMISHNA WA IEBC

Koome ahimiza jopo lililoundwa kuteua makamishna 4 wa IEBC kuzingatia sheria

Koome alikuwa akizungumza kwenye hafla ya kuapishwa kwa Morris Kimuli atakayewakilisha LSK kwenye jopo hilo

Muhtasari

•Uteuzi wa Kimuli ulikuja baada ya Rais Kenyatta kutengua Bi. Dorothy Jemator Kimengench kutoka  kwenye jopo hilo.

•Majina 669 ya watu walioomba nafasi zile yalichapishwa na jopo hilo siku ya Jumanne .

iebc
iebc
Image: Hisani

Jaji mkuu nchini Martha Koome ameagiza jopo litakaloteua makamishna watakaoridhi nafasi zilizowachwa wazi baada ya makamishna wanne wa tume ya IEBC kujiuzulu kati ya mwaka 2017 na 2018 kuzingatia katiba katika utekelezaji wa jukumu lililo mbele yao.

Koome alikuwa akizungumza katika hafla ya kuapishwa kwa Morris Kimuli kama mwanachama wa jopo hilo iliyofanyika katika jumba la mahakama kuu siku ya Ijumaa. Kimuli atakuwa akiwakilisha muungano wa mawakili nchini(LSK) kwenye jopo hilo.

"Kila mtu anawaangalia mteue makamishna wa tume ya IEBC watakaotupatia uchaguzi huru na wa haki" Koome alisema.

Uteuzi wa Kimuli ulikuja baada ya kutenguliwa kwa aliyekuwa ameteuliwa mbeleni, Bi Dorothy Jemator Kimengench na rais Uhuru Kenyatta.

Majina 669 ya watu walioomba nafasi zilizoachwa na Consolata Nkatha, Roselyn Akombe, Paul Kurgat na Margaret Mwachanya yalichapishwa na jopo hilo siku ya Jumanne. 

Mwenye kiti wa jopo hilo, Elizabeth Muli aliapa kuwa watazingatia sheria zote na watatia bidii kumaliza jukumu hilo kwa muda uliopeanwa.