MAUAJI KITENGELA

Mwanamke, 30, akamatwa kuhusiana na mauaji ya msichana wa miaka 8

Inasemekana kuwa simu ya Navity Mutindi ni moja ya zilizotumika na wateka nyara kuitisha malipo ya laki tatu kutoka kwa mama Shantel

Muhtasari

•Navity Mutindi, mhudumu katika duka ya Mpesa, anashukiwa  kudanganya Shantel, 8, kuanguka kwenye mtego wa wateka nyara ambao walimuua.

Marehemu Shantel Nzembi
Marehemu Shantel Nzembi
Image: Hisani

Mshukiwa mwingine mmoja ameshikwa kuhusiana na mauaji ya mtoto, Shantelle, idadi ya waliokamatwa sasa iifikia watatu.

Mwanamke wa miaka 30 kwa jina Navity Mutindi alikamatwa na wapelelezi wa DCI akiwa mafichoni mtaa wa Athi River, kaunti ya Machakos.

Mutindi ambaye inasemekana amekuwa akifanya kazi kwa duka la Mpesa karibu na mahali familia ya Shantel huishi anazuiliwa katika kituo cha polisi cha Kitengela pamoja na washukiwa wengine wawili waliokamatwa siku ya Jumatano.

Inatuhumiwa huenda mshukiwa alidanganya mtoto huyo kuanguka kwa mtego wa wateka nyara ambao walimuua.

Kuna madai kuwa simu yake ni moja ya zilizotumika na watekaji nyara wale kuitisha malipo ya laki tatu kutoka kwa mama mtoto, Christine Ngina.

Siku ya Alhamisi, mahakama ya Kajiado iliamuru wapelelezi kuzuilia kwa siku 10 washukiwa Livingstone Makacha Otengo, 27 , na Francis Mbuthia, 42, ambao walikamatwa siku ya Jumatano ili kumaliza upelelezi.

Iliripotiwa kuwa Otengo ambaye ni mwendeshaji bodaboda mjini Kitengela alikamatwa katika eneo la Orata, Kitengela, akiwa na simu inayoaminika kutumika kuitisha pesa kutoka kwa mamake Shantel.

Mikuhu ambaye alikamatwa mida ya saa tatu usiku siku ya Jumatano anatuhumiwa kutumia kitambulisho chake kuandikisha laini ya Airtel ambayo ilipokea pesa zilizoitishwa.

Hakimu Edwin Mulochi aliashiria washukiwa wazuiliwe katika kituo cha polisi cha Kitengela kwa siku 10 ili wapelelezi wamalize kazi yao.

Iliripotiwa kuwa mwili wa Shantel, 8, ambaye alikuwa mwanafunzi wa daraja la pili ulipatikana ukiwa umetupwa maeneo ya Orata, Noonkopir siku ya Jumatatu baada ya marehemu kukosekana nyumbani tangu Jumamosi wiki iliyopita.

Mama ya marehemu alisema kuwa mwanawe alikuwa ameenda kucheza na rafiki yake aliyetambulishwa kama Sharon na kuonekana kwa mara ya mwisho mida ya saa tisa jioni siku ya Jumamosi.

Upelelezi ulidhibitisha kuwa marehemu hakumpata Sharon na akaamua kuenda kucheza na watoto wengine.

Baadae Bi. Ngina alijaribu kutafuta mwanawe bila mafanikio kisha akapokea simu kutoka kwa namba isiyotambulika akiarifiwa kuwa mwanawe alikuwa mikononi mwao.

Bi Ngina alisema kuwa mwanamke aliyepiga simu alimuagiza kulipa kiwango cha shilingi 300000 ikiwa alitaka kumuona mwanawe akiwa hai tena.

Hata hivyo aliongezea kwa kusema kuwa aliyempigia simu alikuwa akimuita 'Mama Sharon' ingawa yeye ni mama Shantel.