KUZOROTA KWA USALAMA KATIKA VYUO VIKUU

Wanafunzi wa vyuo vikuu kuandamana jijini kulaani ongezeko la visa vya ubakaji na mauaji

Maandamano hayo yanakuja siku chache tu baada ya mwanafunzi katika mwaka wa tatu katika chuo kikuu cha Masinde Muliro kubakwa na kuuliwa kinyama pande za Kakamega.

Muhtasari

•Katibu wa baraza la UPC, Ciff Oketch na ambaye ni mwenyekiti wa muungano wa wanafunzi katika chuo kikuu cha kifundi cha Kenya(TUK) amemwandikia kamanda wa polisi eneo la Nairobi, Augustine Nthumbi, akimuagiza kuwapa wanafunzi ulinzi kwenye maandamano hayo

Tangazo la maandamano
Tangazo la maandamano
Image: Hisani

Wanafunzi wa vyuo vikuu nchini Kenya watakuwa na maandamano ya amani jijini Nairobi siku ya Jumanne.

Baraza ya marais wa vyuo vikuu nchini Kenya(UPC Kenya) imetangaza kuwa wanafunzi wa vyuo vikuu watakuwa wanashiriki maandamano ya amani ili kulaani ongezeko la visa vya ubakaji wa wanafunzi na mauaji ya kikatili.

Katibu wa baraza la UPC, Ciff Oketch na ambaye ni mwenyekiti wa muungano wa wanafunzi katika chuo kikuu cha kifundi cha Kenya(TUK) amemwandikia kamanda wa polisi eneo la Nairobi, Augustine Nthumbi, akimuagiza kuwapa wanafunzi ulinzi kwenye maandamano hayo.

"Maandamano yataanza Uhuru Park, Freedom Corner tupitie jumba la Harambee na yaishie nje ya bunge la kitaifa ambapo tutahutubia wanahabari. Kwa hivyo tunaagiza kupewa ulinzi kutoka ofisini mwako. Mikakati yote ya kuzuia kusambazwa kwa virusi vya Corona itaangaziwa" Oketch alimuandikia Kamanda wa polisi.

Maandamano hayo yanakuja siku chache tu baada ya mwanafunzi katika mwaka wa tatu katika chuo kikuu cha Masinde Muliro kubakwa na kuuliwa kinyama pande za Kakamega.

Mwili wa Macrine Achieng ulipatikana asubuhi ya kuamkia Jumatano wiki iliyopita ukiwa umetupwa kichakani karibu na makazi yake maeneo ya Kefinco.

Marehemu Macrine alikuwa nusu uchi na majeraha katika sehemu mbalimbali za mwili.Iliripotiwa kuwa Macrine alikuwa amebakwa kisha kuuawa kinyama na mwili wake kutupwa mita chache kutoka mahali alipokuwa anaishi. Mshukiwa mmoja, mwanafunzi katika mwaka wa pili, ameweza kukamatwa kufikia sasa huku uchunguzi ukiendelea.

Marehemu Macrine Achieng aliyekuwa mwanafunzi katika chuo kikuu cha Masinde Muliro
Marehemu Macrine Achieng aliyekuwa mwanafunzi katika chuo kikuu cha Masinde Muliro
Image: Hisani

Mwili wa mwanafunzi wa miaka 22 kutoka chuo kikuu cha Egerton ulipatikana ukiwa umetupwa kwenye mto wa Subukia tarehe 7 Desemba mwaka uliopita.

Washukiwa watatu walikamatwa mwezi wa Februari wakituhumiwa kuhusika kwenye mauaji hayo.

Visa vya ubakaiji na mauaji ya wanafunzi wa vyuo vikuu sio swala geni nchini. Angalau kila muhula ripoti za vitendo hivyo huripotiwa kutoka vyuo mbalimbali nchini.