KESI YA TECRA MUNGAI

Mashahidi 3 kwenye kesi ya mridhi wa Keroche watatoa ushahidi kwa kamera-Mahakama

Mashahidi watatu waliokuwa wamefika mahakamani ni pamoja na wauguzi wawili na rafiki mmoja wa Tecra kutoka upande wa Lamu.

Muhtasari

•Bi Tecra aliaga Mei 2 mwaka uliopita alipokuwa anahudumiwa katika hospitali ya Nairobi baada ya kuanguka kutoka kwenye ngazi za nyumba iliyo Lamu.

•Mpenzi wake, Omar Lalli alikamatwa na kutiwa mbaroni ila DPP akaondoa kesi dhidi yake mwezi wa Julai na kuagiza upelelezi zaidi kufanyika.

Tecra na Lali
Tecra na Lali
Image: Maktaba

Mahakama imeamuru kuwa ushahidi wa mashahidi watatu katika kesi ya mauaji ya mrithi wa Keroche, Bi Tecra Mungai utatolewa kwa kamera.

Hakimu mkuu katika mahakama ya milimani, Zainab Abdul, amekubali ombi la upande wa mashtaka kutaka ushahidi huo kutolewa kwa kamera kwa minajili ya usalama wa mashahidi hao.

"Nimekubali ombi la upande wa mashtaka na wahusika wengine ili kulinda usalama wa mashahidi. Sababu zilizopeanwa zinakubalika" hakimu alisema.

Upande wa mashtaka ulikuwa umeomba kesi hiyo ifanyikie mahala fiche kwa kuhofia usalama wa mashahidi.

Mashahidi watatu waliokuwa wamefika mahakamani ni pamoja na wauguzi wawili na rafiki mmoja wa Tecra kutoka upande wa Lamu.Hata hivyo, shahidi mkuu kwenye mauaji hayo, Omar Lali hakufika mahakamani huku akiwakilishwa na wakili wake.

"Nimetoa ombi kesi hii isikizwe kwa kamera kwani mashahidi ni wakazi wa Lamu na wanahofia kwamba usalama wao waweza kuwa mashakani iwapo majina na picha zao zitaonekana kwenye vyombo vya habari" wakili kutoka upande wa mashtaka, Peter Muia aliambia mahakama.

Wakili wa familia ya Tecra alikubali huku akisema kuwa Lamu ni jamii ndogo ambapo mashahidi hutangamana sana na jamii. Hata hivyo alisema kuwa ombi hilo ni kwa mashahidi watatu pekee wanaotoka Lamu.

Bi Tecra aliaga Mei 2 mwaka uliopita alipokuwa anahudumiwa katika hospitali ya Nairobi baada ya kuanguka kutoka kwenye ngazi za nyumba iliyo Lamu.

Mpenzi wake, Omar Lalli alikamatwa na kutiwa mbaroni ila DPP akaondoa kesi dhidi yake mwezi wa Julai na kuagiza upelelezi zaidi kufanyika.

Mashahidi sita waliompeleka marehemu hospitalini, Qusai Omar Lali, Ali Bakari Muhammed, Abdul Lali Omar, Yaya Salim Muhammed, na Mohammed Omar Muhanji wanatarajiwa kutoa ushuhuda wao .

Kufikia sasa mashahidi 11 kati ya 44 walioorodheshwa wametoa ushuhuda wao. Kati ya waliotoa ushuhuda ni mamake marehemu Tabitha Karanja, ndugu ya marehemu James Karanja na kijakazi wao Anne Waithera.