ALIKOSA KUFIKA KWA MARA YA PILI

Seneti: Gavana Wangamati kuamurishwa kufika mbele ya kamati ya afya

Mkutano ulioongozwa na mwenyekiti wa kamati, Seneta Abdullahi Ali uliafikia kutoa wito kwa gavana Wangamati kufika mbele yake baada yake kukosa kufika kwa mara ya pili kujibu maswali kutokanana ukaguzi wa hesabu za matumizi ya pesa za kudhibiti ugonjwa wa COVID 19

Muhtasari

•Wangamati alikuwa amealikwa kufika mbele ya kamati hiyo siku ya Jumanne.

•Seneta wa Bungoma, Moses Wetangula ambaye alikuwa  amehudhuria kikao hichoalisema kuwa seneti haiwezi na sababu za Wangamati kukosa kufika mbele ya seneti.

Gavana wa Bungoma Wycliffe Wangamati
Gavana wa Bungoma Wycliffe Wangamati
Image: JOHN NALIANYA

Kamati ya afya ya Seneti imetoa agizo kwa Gavana wa Bungoma Wycliffe Wangamati kufika mbele yake.

Mkutano ulioongozwa na mwenyekiti wa kamati hiyo Seneta Abdullahi Ali wa Wajir uliafikia kumuamrisha gavana Wangamati kufika mbele yake baada ya kukosa kufika mbele ya kamati hiyo kujibu maswali ya ukaguzi wa hesabu kwa mara ya pili.

Mkaguzi mkuu Nancy Gathungu alikuwa ametilia shaka matumizi ya pesa za kudhibiti ugonjwa wa COVID-19 katika kaunti ya Bungoma na gavana Wangamati alitarajiwa kujibu maswali kuhusiana na matumizi ya pesa hizo.

Wangamati alikuwa amealikwa kufika mbele ya kamati hiyo siku ya Jumanne baada ya mkutano uliokuwa umepangiwa kufanyika tarehe 31 mwezi wa Machi kukosa  kufanyika kwa madai kuwa majibu na hati za kudhibitisha majibu yake hazikuwa zimefikia mkaguzi mkuu.

Kamati hiyo imepinga’ sababu za kishenzi’ na kumsuta gavana Wangamati kwa kupuuza seneti.

Kikao hicho kilihudhuriwa na Seneta Beatrice Kwamboka, Sen Sam Ongeri, Sen Ledama Olekina, Sen Milicent Omanga na Sen Mary Seneta.

Seneta wa Bungoma, Moses Wetangula ambaye alikuwa  amehudhuria kikao hicho kama rafiki wa kamati alisema kuwa seneti haiwezi kukubali vijisababu kuwa Wangamati alikuwa akihudhuria mikutano ya baraza la magavana na mazishi.  

“Tutatekeleza viwango kamili vya sheria ikiwa ni pamoja na uwezekano wa kutoa adhabu na kumpiga faini gavana majukumu ambayo seneti iko na uhuru wa kutekeleza” Wetangula alisema.

Katiba imeruhusu seneti kupitia kamati yoyote kuamuru mtu yeyote kufika mbele yake ili kutoa ushahidi na kujibu maswali. Mtu akikosa kufika mbele ya kamati anaweza tozwa faini isiyozidi shilingi laki tano ama kutolewa amri ya kukamatwa.

Kamati hiyo itakuwa inatoa amri ya gavana wangamati kufika mbele yake siku saba zitakapoisha baada ya kuomba ruhusa kutoka kwa spika.

(Mhariri: Davis Ojiambo)