Maraga amkemea Uhuru kwa ukiukaji wa katiba

Muhtasari

• Maraga alidai kwamba majina ya majaji waliorodheshwa hapo awali yalibadilishwa.

• Mutunga siku ya Jumanne alimshtumu Uhuru kwa kutumia vibaya mamlaka yake ya urais, akitaja utumiaji wake wa nguvu kupita kiasi bila kujali.

Jaji Mkuu mstaafu David Maraga amemkosoa Rais Uhuru Kenyatta kwa kukataa kuapisha majaji sita, akisema utendakazi wake utatiwa doa na mazoea ya kupuuza Katiba bila kujali.

Katika mahojiano kwenye KTN, Maraga alisema Uhuru ana wajibu wa kikatiba kuteua majaji wote walioteuliwa na Tume ya Huduma za Mahakama na kura yake ya turufu kwa majina sita ni sawa na ukiukaji wa sheria.

"Nitamkumbuka kama rais ambaye hajali sheria," alisema alipoulizwa kuhusu kumbu kumbu atakayoiacha rais Uhuru.

Alhamisi iliyopita, Uhuru aliteua majaji 34 na kukataa kuteua wengine sita. Majaji wa Mahakama Kuu Joel Ngugi, George Odunga, Weldon Korir na Aggrey Muchelule, pamoja na hakimu mkuu Evans Makori na msajili wa Mahakama Kuu Judith Omange walikataliwa kwa sababu walidaiwa kuwa na sababu za kimaadili.

Maraga, ambaye aliongoza mahojiano ya JSC na kuteua majaji 41, alisema Rais hakuwasilisha ripoti yoyote mbaya dhidi ya sita hao, hata baada ya kuulizwa kufanya hivyo.

Maraga alidai kwamba majina ya majaji waliorodheshwa hapo awali yalibadilishwa, na kuzua shaka kwamba kukataliwa kulisababishwa na hila.

"Majina yamebadilika. Ninaweza kudhibitisha hilo. Wale ambao walisemekana kutiliwa shaka wengine wameongezwa na wengine kuondolewa kwenye orodha. Ikiwa walikuwa na madai ya kweli, kwa nini wanabadilishwa? Kwanini wanabadilisha majina?" aliuliza.

Uhuru wiki hii amekuwa akishambuliwa na majaji wakuu wastaafu nchini, huku mtangulizi wa Maraga Willy Mutunga akielezea kushindwa kwake kuwaapisha majaji hao sita kama "msimamo hatari na ukiukaji wa sheria".

Mutunga siku ya Jumanne alimshtumu Uhuru kwa kutumia vibaya mamlaka yake ya urais, akitaja utumiaji wake wa nguvu kupita kiasi bila kujali.

Maraga alidai kuwa Rais aliwakataa Odunga na Ngugi kwa sababu ya uamuzi wao ambao ulitia doa mchakato  wa marekebisho ya katiba kupitia BBI.

Wawili hao walikuwa sehemu ya jopo la majaji watano ambalo liliamua kwamba BBI ni kinyume cha katiba.

"Majaji hawa wamehukumiwa bila kusikilizwa ... Sasa, machoni pa umma, hawa ndio majaji wafisadi ambao Rais alikuwa akizungumzia. Huo ndio ujumbe huko nje. Na hiyo inalaani watu hawa bila kupewa fursa ya kusikilizwa, ”Maraga alisema.

Alisema wakati wa uongozi wake kama Jaji mkuu na rais wa Mahakama Kuu, alikataa mapendekezo ya rais kwamba awateue majaji wengine. Alisema hajui ikiwa Rais na mrithi wake Martha Koome walijadiliana na kukubaliana kuhusu majaji wa kuteuliwa na wale wa kuachwa nje. Koome alikuwa katika Ikulu, wakati majaji 34 waliapishwa.

Maraga alilalamika kwamba mazoea ya kutotii maagizo ya korti ya Uhuru na Baraza lake la Mawaziri yalifikia viwango ambavyo havijawahi kutokea.

Ikiwa hali hii itaendelea bila kudhibitiwa, nchi itatumbukia kwenye machafuko na kutokujali kwa sheria, alionya, akimtaka Rais aheshimu Katiba na idara zingine za serikali.