MAUJI YA PADRE KYENGO

Mshukiwa mkuu katika mauaji ya Padri Kyengo akamatwa tena

Mutunga alikuwa amekiri kuhusika kwenye mauaji ya padre huyo huku akisema kuwa ilikuwa kafara ya Illuminati. Alisema kuwa marehemu alikuwa mpenzi wake.

Muhtasari

• Baada ya kuachiliwa huru kwa dhamana ya 300,000, mshukiwa huyo alienda mafichoni na hakwenda mahakamani

• Kisu kinachoaminika kutumika kwenye mauaji na nguo zilizokuwa na damu na bidhaa zingine vilipatikana kwake.

Michael Mutunga
Michael Mutunga
Image: DCI Twitter

Mshukiwa mkuu kwenye mauaji ya padri wa kanisa katoliki yaliyotekelezwa  mwaka wa 2019 amekamatwa kwa mara ya pili.

Michael Mutunga ambaye alihusishwa na mauaji ya Padri Michael Maingi Kyengo mnamo tarehe 8 mwezi wa Oktoba, 2019 alikamatwa tena siku ya Alhamisi katika moja ya vitongoji jijini Nairobi alikokuwa amejificha.

Iliripotiwa kuwa marehemu aliviziwa na kuuawa alipokuwa anatoka sala kuelekea maeneo ya Masinga alikokuwa anahudumu. Washambuliaji walimzika kasisi huyo baada ya kumuua.

Mwili wake ulipatikana ukiwa umefungwa ndani ya gunia na kuzikwa kwenye kaburi lisilo kuwa na kina kirefu mjini Embu.

Marehemu alidhaniwa kuuawa kwa njia ya kunyongwa na kukatwa koo.

Wapelelezi katika mauji hayo  walimkamata Mutunga akiwa na ushahidi ambao ulimhusisha na mauaji hayo.

Kisu kinachoaminika kutumika kwenye mauaji hayo na  nguo zilizokuwa na damu pamoja na bidhaa zingine zilipatiakana kwake.

Mutunga alikuwa amekiri  kuhusika kwenye mauaji ya kasisi huyo huku akisema kuwa ilikuwa kafara ya Illuminati. Alisema kuwa marehemu alikuwa mpenzi wake.

Hata hivyo,  mahakama kuu ya Meru ilimuachilia kwa dhamana ya shilingi laki tatu licha ya ushahidi mkubwa dhidi yake, jambo ambalo liliwashangaza wengi.

Punde baada ya mshukiwa kuachiliwa kwa dhamana alienda mafichoni na hakurejea tena mahakamani kama alivyokuwa ameagizwa. Jambo hili lilipelekea mahakama kuagiza kukamatwa kwake .

Mshukiwa alikamatwa tena baada ya kuwa mafichoni kwa kipindi cha mwaka mmoja.

(Mhariri: Davis Ojiambo)