UNDUGU WA KENYA NA SOMALIA

Somalia yapendekeza maafikiano na nchi ya Kenya

Serikali ya shirikisho la Somalia imesema kuwa iko tayari kurejesha urafiki wa kibiashara na baina ya raia wake ili kuleta mafanikio kwenye nchi hizo mbili.

Muhtasari

‚ÄĘSomalia imesema kuwa iko tayari kurejesha urafiki wa kibiashara na baina ya raia wake ili kuleta mafanikio kwenye nchi hizo mbili.

Rais Uhuru Kenyatta na mwenzake wa Somalia Mohamed Abdullahi Farmaajo. Picha: MAKTABA
Rais Uhuru Kenyatta na mwenzake wa Somalia Mohamed Abdullahi Farmaajo. Picha: MAKTABA

Serekali ya shirikisho la Somalia imependekeza  kuundwa kwa kamati ya pamoja inayohusisha mataifa ya Kenya na Somalia ilikuleta maafikiano ya kidiplomasia kati ya mataifa hayo mawili.

Somalia imesema kuwa iko tayari kurejesha urafiki wa kibiashara na baina ya raia wake ili kuleta mafanikio kwenye nchi hizo mbili.

Kupitia ujumbe kwa wanahabari uliotolewa siku ya Alhamisi, serikali ya Somalia imeridhishwa na hatua ya Kenya kukubali ombi la kufungulia ndege toka Somalia kuingia nchini.

"Hili ni hatua muhimu kuelekea kufanikisha biashara kati ya nchi zetu mbili, maelewano mazuri na usafiri wa raia wa nchi zote mbili" Serikali ya Somalia ilisema.

Somalia ilisema kuwa hatua hiyo ni ishara nzuri ya mwanzo wa mazungumzo yanayotazamia kuhalilisha urafiki kati ya nchi hizo mbili.

"Nchi hizi mbili zenye undugu zimekuwa zikishirikiana katika maswala ya usalama, biashara na utamaduni kwa msingi wa maono moja, ujirani mwema na heshima ya uhuru wa kisiasa" Serikali ya Somalia ilisema.

Hii inakuja wiki moja tu baada ya serikali ya Somalia kulaani vikali jeshi la Kenya almaarufu kama KDF kwa madai kuwa wanajeshi hao wanafanya mashambulio ya angani yanayoumiza na kuua raia wasio na hatia.

Serikali hiyo ilisema kuwa operesheni zinazofanywa na jeshi la KDF zinafanyika kwa njia inayokosa kuwiana na wajibu waliopewa na shirika la umoja wa mataifa kupitia baraza la usalama.