Kijana ashukiwa kuua babake kufuatia mzozo wa kuku

Inadaiwa kuwa alimgonga babake kwa rungu mara kadhaa kichwani huku akidai kufidiwa kuku wake sita ambao alishuku babake alikuwa ameuza

Muhtasari

•Babake kwa hasira alikuwa ametishia kumdunga kwa mishale jambo ambalo lilimfanya kutoroka

•Punde baada ya tukio hilo, kijana huyo alienda mafichoni asijulikane aliko. Wapelelezi  bado wanamtafuta.

Crime scene
Crime scene

Wapelelezi upande wa Londiani, Kericho wanamuwinda kijana mmoja wa miaka 18 anayedaiwa kumuua kinyama babake baada ya kuzozana ju ya kuku waliopotea.

Kijana huyo ambaye ni mwanafunzi wa kidato cha nne katika shule ya upili ya Kapcheplanga anadaiwa kukabiliana na babake, Wilson Kipsoi(50) akitaka kujua mahali kuku wake sita walikuwa kwani alishuku kuwa babake alikuwa amewauza.

Kipsoi kwa hasira alitishia kumdunga mwanawe kwa mishale jambo ambalo lilimfanya kutoroka na kujificha kwa jirani.

Inadaiwa  kuwa kijana yule alirudi nyumbani kwao siku iliyofuata akiwa amejihami na rungu huku akiapa kuwa ni sharti babake angetoa kuku wale.

Alipofika pale nyumbani alimgonga babake kichwani mara kadhaa kwa kutumia rungu huku akidai kufidiwa kuku wake. Shambulio hilo lilimfanya babake kupoteza fahamu na kukimbizwa katika hospitali ya Londiani ambako alifariki akipokea matibabu.

Punde baada ya tukio hilo, kijana huyo alienda mafichoni asijulikane aliko. Wapelelezi  bado wanamtafuta.

Mwili wa marehemu umehifadhiwa katika chumba cha kuhifadhi maiti cha St Joseph huku upelelezi ukiendelea.