Magavana watishia kusimamisha shughuli za kaunti kwa kukosa fedha

Mwenyekiti wa COG Martin Wambora wa Embua amesema kuwa hazina ya kitaifa bado haijaachilia bilioni 102.6 kwa kaunti zote 47

Muhtasari

•Mwenyekiti wa COG Martin Wambora wa Embua amesema kuwa hazina ya kitaifa bado haijaachilia bilioni 102.6 kwa kaunti zote 47 huku mwaka wa fedha ukiwa umebakisha wiki mbili tu kuisha

•Magavana walidai kuwa hazina ya kitaifa haijaachilia pesa kwa kipindi cha miezi sita iliyopita.

mwenyekiti wa baraza la magavana Martin Wambora
mwenyekiti wa baraza la magavana Martin Wambora
Image: Hisani

Magavana wametishia kusitisha shughuli za kaunti wiki ijayo kufuatia ukosefu wa fedha za kuendesha shughuli hizo.

Kupitia baraza la magavana(COG) , viongozi hao wamelalamikia kucheleweshwa kwa pesa za kuendesha shughuli za kaunti  na hazina ya kitaifa jambo ambalo limelemaza kazi na utoaji wa huduma muhimu kwa wananchi.

Mwenyekiti wa COG Martin Wambora wa Embua amesema kuwa hazina ya kitaifa bado haijaachilia bilioni 102.6 kwa kaunti zote 47 huku mwaka wa fedha ukiwa umebakisha wiki mbili tu kuisha na kwa hivyo kupeana hazina ilani kuwachilia pesa kabla ya siku ya Ijumaa la sivyo shughuli za kaunti zitasitishwa.

“Iwapo hazina ya kitaifa haitawachilia pesa , kaunti hazitaweza kupeana huduma za kimsingi na kwa hivyo italazimu kusimamishwa kwa huduma ama kufungwa kabisa kwa kaunti kuanzia Juni 24 Wambora alisema.

Gavana huyo wa Embu alikuwa akizungumzia wanahabari katika makao maku ya COG jijini Nairobi siku ya Jumapili akiandamana na gavana James Ongwae wa Kisii na James Nyoro wa Kiambu.

Magavana walidai kuwa hazina ya kitaifa haijaachilia pesa kwa kipindi cha miezi sita iliyopita. Wambora alisema kuwa hazina ilikuwa imekiuka katiba na ratiba yake.