Afisa wa polisi asimulia masaibu ya siku 17 ndani ya msitu wa Boni

Muhtasari

• Wakati msafara ulipokuwa ukipita kwenye barabara ya Bodhei katika eneo la Baure, moja ya gari lao likapita juu ya bomu la kutegwa ardhini na kulipuliwa.

• Wakati wanamgambo walikuwa wakifyatulia risasi msafara wao, Kiunga alitorokea usalama kwenye kichaka.

• Aligundua baadaye kwamba alikuwa amepigwa risasi mkononi na paja.

Konstebo Norman Kiunga akiwa hospitalini na Waziri wa Mambo ya Ndani Fred Matiang'i na Inspekta mkuu wa polisi Hilary Mutyambai jijini Nairobi mnamo Juni 4 baada ya kuhamishwa kutoka Lamu. Picha: WIZARA YA NDANI
Konstebo Norman Kiunga akiwa hospitalini na Waziri wa Mambo ya Ndani Fred Matiang'i na Inspekta mkuu wa polisi Hilary Mutyambai jijini Nairobi mnamo Juni 4 baada ya kuhamishwa kutoka Lamu. Picha: WIZARA YA NDANI

Asubuhi ya Mei 18, Norman Kiunga alikuwa amevalia sare yake, alibeba bunduki ya Negev na bastola na alijiunga na maafisa wenzake wa Kikosi cha kushika doria mpakani.

Rais Uhuru Kenyatta alitarajiwa katika Bandari ya Lamu siku mbili baadaye na kikosi katika Msitu wa Boni kilikuwa imara kuzuia shambulio lolote la wanamgambo wa al Shabaab.

Kikosi hicho kilikuwa na ripoti za kijasusi kwamba wanamgambo hao walikuwa wameonekana katika eneo hilo na walikuwa wakipanga shambulio kabla ya ziara ya Uhuru.

Wakati msafara huo ulipokuwa ukipita kwenye barabara ya Bodhei-Kiunga katika eneo la Baure, moja ya gari lao likapita juu ya bomu la kutegwa ardhini na kulipuliwa.

Katika mkanganyiko uliofuata, wanamgambo hao walianza kufyatulia risasi kikosi cha maliokuwa wakishika doria. Maafisa sita walipoteza maisha na wengine kadhaa walijeruhiwa.

Wakati wanamgambo walikuwa wakifyatulia risasi msafara wao, Kiunga alitorokea usalama kwenye kichaka kilichokuwa karibu. Aligundua baadaye kwamba alikuwa amepigwa risasi mkononi na paja.

Iliashiria mwanzo wa masaibu na mateso ya siku 17 ya Kiunga katika Msitu mpana wa Boni. Msitu huo umeenea hadi Somalia na umejaa tembo, nyati, nguruwe wa mwituni miongoni mwa wanyama wengine hatari.

Akiwa amejaza mkoba wake kwa maji, chakula, vifaa vya matibabu na vitu muhimu vya msituni, Kiunga alikimbia hadi akashindwa kwenda tena na akasimama chini ya mti ili ajipake vidonda. Alikaa usiku msituni akihisi  maumivu makali.

Wakati huo huo, maafisa wengine sita ambao walikuwa wamejificha msituni na hapo awali walidhaniwa kuuawa walipata njia kurejea kambini mwao saa kadhaa baadaye.

Mara kwa mara, Kiunga aliweza kusikia milio ya risasi, ambayo ilimfanya aogope hata zaidi. Lakini aliendelea kusonga mbele. Alitembea  na wakati mwingine aliweza kuona Bahari Hindi.

Kadri siku zilivyozidi kusonga, Kiunga alimaliza chakula alichokuwa nacho. Wakati chakula kiliisha kabisa, alikula matunda ya mwituni na kuishi zaidi ya majuma mawili msituni.

Siku kadhaa baadaye, alipata mto ambapo alichukua wakati wake kuoga na kuhisi nafuu kidogo.

“Nilikuwa nikikutana na wanyama pori na watu wengine, lakini sikuwa na imani yeyote. Nilikimbilia na kujificha kutoka kwao. Mafunzo yangu yalichangia sana uzoefu wangu na uvumilivu, ”alisema akiwa hospitalini Nairobi.

Wakati wa kutisha zaidi kwa Kiunga ni wakati wa kufuata mkondo wa mto kwenda juu, alikutana na wapiganaji 30 wa Alshabaab wakiooga.

Kiunga alipanda na kujificha juu ya mti na kusubiri waondoke.

Alikuwa na uhakika kwamba mto huo ungemfikisha kwenye kambi yake au kituo cha polisi, kwani huduma nyingi za umma na za kibinafsi zimejengwa kando ya mito.

Huku vidonda vyake vikiwa bado vimefura, alitembea kwenda juu hadi kambi ya Basuba GSU mnamo Juni 2 ambapo wenzake walishtuka na kufurahi sana kumwona. Alikuwa dhaifu na amekonda.

Kiunga alikuwa bado na risasi iliyokwama kwenye paja lake la kulia na jeraha karibu na kiwiko. Afisa huyo alikuwa na bunduki yake ya Negev bila risasi na bastola yenye risasi 11.

Katika siku chache baada ya kuishiwa risasi za bunduki yake na alikuwa na bastola yake tu, aliendelea kuomba kwamba asikutane na adui yeyote mwenye silaha.

Baada ya kurejea katika kituo hicho, alishughulikiwa na kikosi cha matabibu kabla ya kuhamishwa kwenda Nairobi kwa matibabu zaidi.

Mjini Nairobi, Waziri wa Mambo ya Ndani Fred Matiang’i, Inspekta Jenerali wa Polisi Hilary Mutyambai na Naibu Inspekta Jenerali wa Polisi Noor Gabow walimtembelea hospitalini ambapo walimpongeza kwa ujasiri wake.

"Kama kawaida tulitarajia mashambulio kama hayo kutokea lakini kilichofuata ni ulikuwa mtihani mgumu sana," Kiunga alisema.