Francis Atwoli Road

"Hainiumi!" Atwoli alaani walioteketeza bango la ishara la 'Francis Atwoli Rd'

Tukio hili linakuja wiki mbili tu baada ya Atwoli kutangaza kuwa kamera za CCTV zilikuwa zimewekwa kulinda ishara

Muhtasari

•Mwanaharakati Boniface Mwangi alikuwa ameapa kuliharibu siku chache baada ya kuwekwa

•“Kuangusha ishara ya barabara ambayo imeandikwa jina langu hainiumi. Tendo hilo litawinda milele wale ambao walitekeleza. Inawasaidia vipi? Unalalaje usiku ukijua ni wewe ulifanya?Atwoli aliandika.

Ishara ya barabara ya Atwoli yateketezwa
Ishara ya barabara ya Atwoli yateketezwa
Image: Hisani

Katibu mkuu wa muungano wa kitaifa wa wafanyikazi (COTU) Francis Atwoli amekashifu aliyeteketeza bango la ishara ya barabara la ‘Francis Atwoli Road’ mtaani  Kileleshwa.

Kupitia mtandao wa Twitter, Atwoli amesema kuwa tendo hilo ambalo lilifanyika usiku wa kuamkia Jumanne halimuumi hata kidogo huku akisema kuwa wateketaji hao hawatapata amani.

“Kuangusha ishara ya barabara ambayo imeandikwa jina langu hainiumi. Tendo hilo litawinda milele wale ambao walitekeleza. Inawasaidia vipi? Unalalaje usiku ukijua wewe ni mteketezaji?Atwoli aliandika.

Tukio hili linakuja wiki mbili tu baada ya Atwoli kutangaza kuwa kamera za CCTV zilikuwa zimewekwa kulinda ishara hiyo baada ya mtu ambaye hakujulikana kuiangusha.

Mwanaharakati Boniface Mwangi alikuwa ameapa kuharibu ishara ile siku chache baada ya kuwekwa. Hata hivyo,  alipofika pale baada ya kurudi nchini kutoka nchi ya Luxemborg, alidai kuwa Atwoli alikuwa ameajiri wahuni kuilinda ishara ile.

Atwoli amesisitiza kuwa jina lake linajulikana kote ulimwenguni na hahitaji ishara ya barabara kujitambulisha.

“Jina langu limeenea kote ulimwenguni na ishara ya barabara haihitajiki ili watu wajue Francis Atwoli ni nani. Jina langu litadumu kutokana na kazi kubwa ya kujitolea kutetea wafanyakazi wa Kenya na duniani kote ambayo nimeifanya” Alisema Atwoli.

Amesema kuwa ishara hiyo ilikuwa tu ishara ya heshima kwake kutoka kwa kaunti ya Nairobi huku akiwashukuru kwa kutambua kazi yake.

(Mhariri Davis Ojiambo)