Vipi kuhusu 8M waliotuchagua? Ruto akosoa tamko la rais

Hakuna kijana, mwanamke, mwanaume kati ya milioni nane walioamka mapema na kuchagua Rais Kenyatta na William Ruto anayestahili kuungwa mkono?? Ruto aliandika

Muhtasari

•“Sawa tu! Tutajipanga na usaidizi wake Mungu” Ruto alisema.

•Ruto alikuwa akitoa hisia zake kupitia mtandao wa Twitter  kuhusiana na ripoti ya gazeti la The Star ambayo ilidai kuwa Rais Kenyatta angemchagua mmoja wa viongozi wa mrengo wa NASA kuriidhi kiti chake.

Naibu rais William Ruto
Image: Maktaba

Vipi kuhusu ‘thurakus’, wale wa kikosi cha kumera kumera(Kutokea kutokea), sisi wote milioni nane? Ni swali ambalo naibu rais William Ruto ameuliza hadharani kutokana na chaguo la rais la atakayeridhi kiti chake.

Ruto alikuwa akitoa hisia zake kupitia mtandao wa Twitter  kuhusiana  na ripoti ya gazeti la The Star ambayo ilidai kuwa Rais Kenyatta atachagua mmoja wa viongozi wa mrengo wa NASA kuriidhi kiti chake.

 The Star ilikuwa imechapisha kuwa Rais Kenyatta alidai kuwa angemchagua mmoja kati ya Raila Odinga, Kalonzo Musyoka, Musalia Mudavadi na Moses Wetangula  iwapo wangeungana tena na kukubaliana nani kati yao angepeperusha bendera.

Naibu Rais ambaye alionekana kustaajabishwa na ripoti hiyo alitaka kujua hatima ya zaidi ya wapigaji kura milioni nane ambao walimpigia Rais Kenyatta kura mwaka wa 2017.

“EUCHO!!! NGAI FAFA MWATHANI!! vipi kuhusu ‘thurakus’, wale wa kikosi cha kumera kumera (kutokea kutokea), sote milioni nane?? Hakuna  kijana, mwanamke, mwanaume kati ya milioni nane walioamka mapema na kuchagua Rais Kenyatta na William Ruto anayestahili kuungwa mkono?? Ruto aliandika.

Aliendelea kusema kuwa atajipanga kwa usaidizi wake Mungu ili kuweza kunyakua ushindi mwaka ujao.

“Sawa tu! Tutajipanga na usaidizi wake Mungu” Ruto alisema.

Siku ya Jumatatu, Rais aliwaagiza wakuu wa muungano wa NASA kuungana ili waweze kuunda serikali baada yake kustaafu mwaka ujao. Matamshi  hayo ya rais yaliashiria kuwa atakuwa akimpinga naibu rais kwenye uchaguzi mkuu mwaka ujao.

Kutokana na hayo, Ruto ambaye hajakuwa kwenye mahusiano mema na rais tangu salamu za ‘handshake’ kati ya rais na kinara wa ODM Raila Odinga alihisi kwamba ametemwa nje.

Rais aliwapokea viongozi toka Ukambani kwenye ikulu siku ya Jumatatu. Kati ya waliohudhuria mkutano huo ni pamoja na Kalonzo Musyoka, Charity Ngilu na Alfred Mutua.

Kwenye mkutano huo, rais alisihi viongozi wote kushirikiana pamoja ili kuwezesha taifa la Kenya kuwa taifa la mapato ya kati kufikia mwaka wa 2030.

Rais alisema kuwa ameweza kuzindua miradi mingi katika muhula wa pili kwani aliamua kuweka siasa kando na kuzingatia maendeleo .