Dereva aliyemuua binti wa naibu mkuu wa polisi azuiliwa

Muhtasari

• Mtuhumiwa aliendesha gari akienda nyuma katika njia ya hatari na kumfinya Nelly Waithera kwa gari lingine.

Mshukiwa Patrick Macharia Magu
Mshukiwa Patrick Macharia Magu

Dereva wa matatu ambaye anadaiwa kumuua binti wa Naibu Inspekta Jenerali wa Polisi kwa kuendesha gari vibaya siku ya Jumatatu alizuiliwa kwa siku nne zaidi akisubiri uchunguzi.

Patrick Macharia alizuiliwa na hakimu mkazi mwandamizi Esther Kimilu katika kituo cha polisi cha Central baada ya ombi la upande wa mashtaka.

Katika hati ya kiapo, Konstebo Peter Ndirangu alisema mshukiwa alikamatwa Juni 17. Macharia anatuhumiwa kumuua Nelly Waithera, 25, binti wa naibu Inspekta mkuu wa polisi Edward Mbugua.

Ndirangu alisema wakati huo, Macharia alikuwa akiendesha matatu ya KMO Sacco katika makutano ya barabara ya Tom Mboya na ile ya Murang’a.

"Mtuhumiwa aliendesha gari akienda nyuma katika njia ya hatari bila tahadhari kwa watumiaji wengine wa barabara na kumfinya mtu aliyekuwa akitembea kwa miguu kwa jina Nelly Waithera kwa gari lingine," afisa huyo aliiambia korti.

Alisema Waithera alipata majeraha mabaya na alikimbizwa katika Hospitali ya Kitaifa ya Kenyatta, ambapo alifariki.

Ndirangu ameongeza kuwa Macharia, baada ya kugundua kosa lake, aliacha basi hilo eneo la tukio na kukimbia kukwepa kukamatwa.

Alifuatwa na kukamatwa katika barabara ya University Way na kuzuiliwa katika kituo cha polisi cha Central.

"Kitendo cha mshukiwa kutoroka kutoka eneo la tukio ni ishara tosha kwamba hakuwa na nia ya kuripoti ajali hiyo au kujiwasilisha kwa kituo chochote cha polisi au afisa wa polisi," hati ya kiapo inasoma.

Mwili wa Waithera ulipelekwa kwenye chumba cha kuhifadhi maiti cha  Chuo Kikuu cha Kenyatta.

Polisi walisema kuwa uchunguzi haujakamilika kwani wanasubiri matokeo ya upasuaji wa mwili na taarifa muhimu za mashahidi wa upande wa mashtaka kwa hivyo suala hilo halingeweza kuwasilishwa kortini siku ya Ijumaa.

Ndirangu alisema kuwa Macharia ni hatari na huenda akatoroka ikiwa ataachiliwa kwa dhamana.

Waithera alikuwa akivuka kutoka barabara ya Tom Mboya siku ya Alhamisi saa mbili asubuhi alipokumbana na mauti.

Kesi hiyo itatajwa mnamo Juni 24