UHALIFU MACHAKOS

Machakos; Umati wapiga na kuua watekaji nyara waliomuibia ajuza Sh350000

Veronica na mumewe walitoa nusu milioni kwenye, wakalipa wakili Sh150,000, Veronica akabeba 350,000 zilizosalia

Muhtasari

•Baada ya kufika Kaloleni, Veronica aliabiri pikipiki ila safari yao ikakatizwa na gari nyeupe lililokuwa linakuja mbio baada ya umbali wa mita mia mbili tu.

•Mawe, mateke na ngumi zilienea katika eneo hilo la tukio na kuwaacha wawili kati ya wahalifu hao watatu wakiwa wamekata roho.

crime
crime

Watekaji nyara wawili walipigwa hadi kufa na raia wenye ghadhabu baada ya kuteka nyara na kumuibia pesa  ajuza mmoja  upande wa Machakos.

Kulingana na ripoti iliyoandikwa na DCI, majambazi watatu waliteka nyara mwanamke   aliyekuwa amebeba kitita cha shilingi 350, 000, wakampora pesa zile kisha kumtupa  nje.

Imeripotiwa kuwa Veronica Kwanza Kiilu, 60, pamoja na mume wake Jackson Mulinge, 72, walikuwa wametoa shilingi nusu millioni kwenye benki moja mjini Machakos na kutumia Sh150,000 kati ya hizo kulipa wakili.

Hata hivyo, haijabainishwa kwa nini walimlipa wakili huyo anayefanya kazi mjini Machakos.

Baada ya hapo, Mulinge alisalia mjini Machakos wakati bibiye aliabiri matatu kuelekea maeneo ya Kaloleni, Mua Hills huku akiwa amebeba  Sh350,000 zilizobakia.

Baada ya kufika Kaloleni, Veronica aliabiri pikipiki ila safari yao ikakatizwa na gari nyeupe lililokuwa linakuja mbio baada ya umbali wa mita mia mbili tu.

Wanaume wawili walitoka nje ya gari na kumyakua ajuza huyo kisha kumrusha kwenye kiti cha nyuma cha gari hilo na kisha kuenda mbio kuelekea madukani ya Muthwani.

Walipochukua Sh350,000 ambazo Bi Veronica alikuwa amebeba, walimtupa nje kisha kutoweka mbio kwa gari lao bila kujua siku yao ya arubaine ilikuwa imewadia.

Waendeshaji bodaboda ambao walikuwa washapokea ripoti ya uvamizi huo walikatiza safari ya gari lao walipokuwa wanakaribia kufika eneo la Ndovoini.

Kwa hasira, wanabodaboda wakishirikiana na raia wengine waliwafurusha kutoka ndani ya gari na kuwapiga bila huruma yoyote. 

Mawe, mateke na ngumi zilienea katika eneo hilo la tukio na kuwaacha wawili kati ya wahalifu hao watatu wakiwa wamekata roho.

Hata hivyo, mmoja wao ambaye anadhaniwa kuitwa Katu Nzalu alinusurika kifo baada ya kuweza kutoroka na kutokomea.

Redio ya mawasiliano na simu tatu ni baadhi ya vitu vilivyopatikana.

Maafisa wa polisi upande wa Machakos wanaendelea kumtafuta mshukiwa aliyeenda mafichoni.